Siku
hazigandi. Nathubutu kusema hivyo kwani Desemba 12, 2013 ndiyo siku
ambayo nguli Ramadhan Mtoro Ongala ‘Dk, Remmy’ alitimiza miaka saba tangu aiage dunia. Dk. Remmy alifariki usiku wa kuamkia Jumatatu,2010 nyumbani kwake Sinza jijini Dar es Salaam, baada ya
kusumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya kisukari. Akawaacha wapenzi
wake wa muziki wa dansi na Injili pia wananchi kwa ujumla katika dimbwi
la majonzi yasiyosahaulika kutokana na tungo za nyimbo zake, ambazo hadi
leo zinarindima katika vituo vingi vya redio hapa nchini na hata nje ya
mipaka yetu.
Dk. Remmy alikuwa wa kwanza kupata ujasiri wa kukemea ngono zembe,
akatunga wimbo wa Mambo kwa soksi, lakini jamii ikambeza kwamba wimbo
huo haukuwa na maadili mema. Baadaye viongozi wa Serikali na dini na
watu kwa jumla walielewa nini alichokuwa akisema Dk. Remmy. Wakaanza
kuhubiri majukwaani hadhari hiyo.
Wakati wa uhai wake, Dk. Remmy alijipatia umaarufu katika jiji la Dar
es Salaam, hususani maeneo ya Sinza. Alikuwa na gari lake dogo soloon
lililokuwa la aina yake ambako kokote lilikopita watu walilishangaa.
Nyuma ya gari hilo kulikuwa na maneno, ‘Baba yako analo’?
Historia
ya maisha ya Dk. Remmy inaeleza kwamba mara Dk. Remmy Ongala
alipozaliwa, wazazi wake walimuita Ramazani Mtoro Ongala. Alizaliwa
mwaka 1947 katika Mkoa wa Kivu, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Familia
yake iliishi katika eneo lililoitwa Kindu, si mbali kutoka mpakani na
Tanzania. Baba yake alikuwa mwanamuziki mashuhuri na mpiga ngoma kwa
kutumia mikono na mbira. Baada ya kuzaliwa haikuchukua muda mrefu
familia yake ilihamia katika mji wa Kisangani huko huko DRC.
Ipo
habari kwamba kabla ya kuzaliwa, mama yake alipata ujauzito mara mbili,
lakini kwa bahati mbaya kila alipojifungua, watoto walifariki.
Alipopata ujauzito mara ya tatu alienda kwa mganga wa kienyeji kumuomba
ushauri afanye nini ili mtoto atakayezaliwa asiage dunia.
Bila
kusita, mganga wa kienyeji akampa ushauri. Akamwambia kwanza safari hii
asiende kujifungulia hospitali, bali akajifungulie porini. Pia alipewa
ushauri kwamba mtoto akishazaliwa asije akamkata nywele zake. Yote hayo
yalitendeka na ndiyo kisa cha Dk. Remmy kutokata nywele hadi alipozidiwa
na maradhi yaliyomfanya aokoke, na ndipo aliponyoa nywele zake akiwa
nchini Tanzania.
Mwenyewe
aliwahi kusema kwamba mwanzoni alikuwa anajisikia aibu sana kuwa na
nywele ndefu namna ile, hadi baadaye jina na taswira ya mfalme wa reggae
ulimwenguni, Bob Marley ilipopata umaarufu nchini DRC, ndipo
alipoipenda staili ile ya nywele kwani hata watu wengine pia walianza
kuikubali na kuionea fahari.
Pia
inasemekana Remmy alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya mbele, kitu
ambacho kwa imani ya kabila lao, kilichukuliwa kama ishara ya baadaye
kuja kuwa mganga wa kienyeji. Ingawa utabiri huo haukutimia, inasemekana
huo ndiyo ukawa mwanzo wa yeye kujulikana hapo baadaye kama Dokta Remmy
Ongala.
Baba
yake ndiye aliyeanza kumfunza masuala ya muziki tangu akiwa mdogo
kabisa. Jambo hilo lilimfanya aamini kabisa kwamba kama jinsi ambavyo
watu wengine wamezaliwa kuwa madaktari, wanasheria, waalimu, wakulima
n.k, yeye alizaliwa ili awe mwanamuziki.
Kwa
bahati mbaya baba yake huyo alifariki dunia na kumuacha Dk. Remmy akiwa
na umri wa miaka sita, akiwa tayari ameshaanza shule. Lakini kutokana
na ukosefu wa fedha na kwa sababu mama yake hakuweza kuendelea kumlipia
karo, ilibidi aache shule.
Kwenye
miaka ya1960, Remmy alikuwa ameshajifunza mwenyewe kupiga gitaa. Mwaka
1964 ulikuwa si mwaka mzuri kwake kwani mama yake mzazi alifariki dunia;
jambo ambalo lilimuacha Dk. Remmy na mzigo wa kuwalea wadogo zake.
Bila
elimu na ujuzi mwingine wowote, alilazimika kuanza kujitafutia riziki
kupitia muziki. Ujuzi wake wa kupiga gitaa uliongezeka kwa kasi ya
ajabu, kitu ambacho kilimwezesha kutumbuiza kwa kupiga ngoma na gitaa
katika hoteli nyingi na sehemu mbalimbali nchini DRC akiwa na bendi yake
iliyokuwa imesheheni vijana wenzake iliyoitwa Bantu Success.
Kwa
miongo kadhaa iliyofuata, Dk. Remmy alizunguka sehemu mbalimbali za
Congo akiambatana na bendi kadhaa maarufu za wakati huo nchini humo,
zikiwamo Success Muachana na ile ya Grand Mickey Jazz nchini Uganda.
Japokuwa
Dk. Remmy alijifunza mwenyewe kupiga gitaa, lakini aliwahi kukiri
kwamba muziki wa kutoka Cuba ambao wakati huo ulikuwa unaanza kujipatia
umaarufu barani Afrika, ulimsaidia kupata staili za pekee katika upigaji
gitaa. Kwa upande wa uimbaji anasema uimbaji wa Joseph Kabasele ‘Grand
Kale’ na ule wa Franco ulimsaidia kupata staili yake ya uimbaji kama
tulivyoizoea kusikia enzi za uhai wake.
Maisha yake nchini Tanzania
Mwaka 1978 Dk. Remmy aliingia jijini Dar es Salaam baada ya kuitwa na
mjomba wake, Kitenzogu Makassy, ili ajiunge katika bendi maarufu ya
wakati huo ya Orchestra Makassy iliyokuwa chini ya uongozi wa mjomba
wake huyo.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa maisha ya Dk. Remmy nchini Tanzania. Akiwa
na bendi ya Orchestra Makassy, alitunga wimbo wake wa kwanza
uliojulikana kama Siku ya Kufa, wimbo ambao aliuandika kumkumbuka rafiki
yake aliyefariki dunia.
Wimbo huo ulianza kumpatia umaarufu mkubwa na kujulikana kwa haraka ndani na nje ya nchi. Mzee
Makassy aliamua kuihamishia bendi yake nchini Kenya, kitendo
kilichomfanya Dk. Remmy ajiunge na bendi ya Matimila baada ya kudumu
katika bendi ya Orchestra Makassy kwa takriban miaka mitatu hivi.
Jina
la bendi hiyo ya Matimila lilitokana na jina la kijiji kimoja kilichoko
kusini mwa Tanzania. Kujiunga kwa Dk. Remmy katika bendi ya Matimila,
kulimwongeazea umaarufu katika anga za muziki nchini Tanzania wakati
huo. Chini ya uongozi wake, Dk. Remmy aliisuka upya bendi hiyo na
kuibadilisha jina ikaitwa Orchestra Super Matimila.
Miaka
iliyofuata Watanzania walishuhudia umaarufu wa Dk. Remmy ukiongezeka
kutokana na mashairi ya nyimbo zake, ambayo yaliegemea katika
kuzungumzia mambo halisi ya kijamii kama vile umasikini, afya, siasa,
majanga ya Ukimwi nk.
Mafanikio
ya Dk. Remmy na kundi lake zima la Super Matimila hayakuishia nchini
Tanzania, kwani katika miaka ya mwishoni mwa 1980 walianza kujipatia
umaarufu nje ya Tanzania na Afrika.
Dk.
Remmy aliwahi kusema kwamba kupata mialiko ya nje lilikuja kama mchezo
tu. Alimpa kaseti yenye nyimbo zao rafiki yake mmoja Mzungu aliyekuwa
akiondoka nchini Tanzania kurejea kwao Uingereza.
Rafiki
yake huyo alipofika huko aliwapatia jamaa wa World of Music, Arts and
Dance (WOMAD) ambalo ni shirika linalopandisha chati wanamuziki na
wasanii mbalimbali kutoka katika nchi za Dunia ya Tatu. Walivutiwa na
nyimbo zao na hivyo kuwapa Super Matimila mwaliko kushiriki katika
maonesho yao barani Ulaya mwaka 1988.
Baada
ya kureja nchini, bendi ya Super Matimila ilitoa albamu yenye jina la
Nalilia Mwana ikiwa na mkusanyiko wa nyimbo zao zilikuwemo nyimbo
zilizopendwa sana kama vile Ndumila Kuwili na Mnyonge Hana Haki.

Dk.
Remmy aliwahi kufafanua kuwa wimbo maarufu ya Kipenda Roho, aliuimba
mahsusi kwa ajili ya mkewe, ambaye ni Mzungu Mwingereza, ambaye wakati
huo tayari walikuwa wameshazaa watoto watatu.
![]() |
Aziza Ongala Binti wa Remmy Ongala |
![]() |
Kali Ongala Mtoto wa remy Ongala |
Mwaka
1990, Remmy na bendi yake ya Super Matimila walirejea tena katika
studio za Real World ambako walirekodi albamu nyingine yenye nembo ya
‘Mambo’ ambayo ilikuwa na wimbo kama huo wa Mambo ambao aliuimba kwa
lugha ya Kiingereza na kuweza kukidhi kiu ya wapenzi wake wasiojua
Kiswahili. Nyingine ni pamoja na No Money, No Life na One World.
Umaarufu
wake ulizidi kung’ara mwaka 1990 alipotoa wimbo wa Mambo kwa Soksi
ingawa baadhi ya watu waliupinga kwa kusema kwamba haukuwa na maadili
ingawa kimsingi alikuwa anawaasa watu, hususani vijana kutumia kondomu
ili kuepukana na maambukizi ya Ukimwi.
Akiwa
Super Matimila, Dk. Remmy alitoka na nyimbo nyingi zikiwamo za Bibi wa
Mwenzio, Kipenda Roho, Asili ya Muziki na Ngalula. Nyingine ni Mwanza,
Mama Nalia, Harusi, Hamisa, Mnyonge Hana Haki, Ndumila Kuwili na Mtaka
Yote, ambazo zilimuongezea sifa kubwa kutokana na maudhui yaliyokuwa
yakiigusa jamii.
Baadaye
Dk. Remmy alianza kusumbuliwa na maradhi ya kisukari yaliyomfanya
aachane na muziki wa dansi kwa madai ya kwamba umejaa mambo mengi ya
kishetani. Baada ya kuokoka, akatubu dhambi zake na akaanza kumuimbia
Bwana.
Kabla
ya kifo, Dk. Remmy alitoa albamu yake ya injili aliyoiita Kwa Yesu Kuna
Furaha.
Dk. Remmy alikuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha albamu
yake ya pili, lakini Mungu akampenda zaidi usiku wa kuamkia Jumatatu,
Desemba 12,2010 nyumbani Sinza.
Eneo hilo alilokuwa akiishi lilipewa jina la Sinza kwa Remmy kutokana na umaarufu wake.
Mungu aiweke roho yake Mahali Pema Peponi, Amina.
By: Kiyungi
By: Kiyungi
Miaka Saba (7) Tangu kifo Nguri wa muziki wa dansi Dkt. Remmy Ongala
Reviewed by CONVIDA FUNERAL HOME COMPANY LIMITED
on
4:37 PM
Rating:

No comments:
Post a Comment