Abeid Karume 1964 |
Bwana Abeid Amani Karume alizaliwa na ndugu wanne wa baba mmoja na mama mmoja ambao ni wanaume wawili na wanawake wawili. Lakini wote walifariki kutokana na maradhi mbalimbali na kubaki yeye peke yake. Kwa upande wa mama mmoja, Abeid Amani Karume alizaliwa na ndugu watatu, wanawake wawili na mwanaume mmoja ambao ni Asha, Shumbana na Othman. Baba yake mzazi Abeid Amani Karume alifariki dunia mwaka 1909 wakati Abeid Amani Karume akiwa na umri wa miaka minne. Bwana Abeid Amani Karume alipata elimu ya Kurani na alianza masomo ya msingi katika skuli ya Mwera mwaka alofariki baba yake wa 1909, ambapo darasa lao lilikuwa la kwanza kuifungua skuli hiyo.
Katika mwaka 1913 wakati akiwa na umri wa miaka 8 mama yake mzazi
alimpeleka mjini Unguja kuendelea na masomo. Huko aliishi na mjomba wake
aliyekuwa Sajenti katika jeshi la polisi la King African Rifle (KAR).
Kwa bahati mbaya muda wake wote wa masomo ulikuwa miaka mitatu. Akiwa
mjini Zanzibar Abeid Karume alipata marafiki kadhaa na kuvutiwa mno na
harakati za bandari ya Zanzibar.
Kwa wakati huo, bandari ya Zanzibar ndiyo iliyokuwa kubwa Afrika
mashariki. Pia Zanzibar, ilikuwa ndiyo kituo kikuu cha biashara katika
eneo zima la Afrika mashariki na Maziwa Makuu.
Meli za mataifa ya nje hasa Marekani, Uingereza, Ufaransa na
Italia zilitia nanga bandarini Zanzibar kupakia na kupakua bidhaaa
mbalimbali. Pia meli nyingi zilifika Zanzibar kuchukua maji safi ya
kunywa yatokayo katika chemchem ya Mwanyanya. Meli hizo zilitoa ajira ya
muda ya kusafisha mashine na kupangusa moshi. Mara nyingi mabaharia wa
meli hizo waliajiri watoto kuwachukulia vikapu vya kununulia vyakula
sokoni na kuwalipa ujira mdogo.
Kwa vile alipendelea kazi ya ubaharia, Abeid Amani Karume
alifuatana na bwana mmoja aitwae Juma hadi bandarini. Alijumuika na
watoto kadhaa waliofuata ajira ya muda huko bandarini. Ajira ya muda
aliyoipata Karume huko bandarini ilimfanya akutane na mabaharia wa nchi
mbalimbali na hivyo kuvutiwa na uzuri wa maisha ya ubaharia ya kusafiri
na kuona nchi na watu mbalimbali. Hali hiyo ilimfanya Karume azidi hamu
na ari ya kutafuta kazi ya ubaharia na kumuomba mama yake ruhusa ya
kufanya kazi melini. Mwanzoni mama yake mzazi alikataa shauri hilo.
Lakini baadaye alikubali ombi hilo baada ya kufahamishwa kuwa meli
atakayofanyakazi mwanawe haitosafiri mbali na itatia nanga bandarini
Zanzibar mara kwa mara.
Katika mwaka 1919 Abeid Amani Karume alipeleka barua ya kuomba
kazi melini lakini alikataliwa kwa vile alikuwa na umri mdogo wa miaka
14. Hata hivyo hakuvunjika moyo na hakurudi Mwera kwa mama yake bali
alimtembelea mara kwa mara. Alijiunga na timu za masumbwi na mpira wa
miguu na kujuana na watu mbalimbali.
Kwa wakati huo timu za mpira wa miguu zilizojulikana Unguja
zilikuwa ni timu ya skuli ya Kiungani iliyoanzishwa na Mwalimu Augostino
Ramadhani na John Majaliwa. Mara nyingi timu hiyo ilishindana na timu
ya watumishi serikalini. Baadaye kuliundwa timu nyengine za mpira wa
miguu ambazo ni Vuga Boys, New Generation, United Service na New Kings.
Karume alijiunga na timu ya New Generation na kucheza nafasi ya mstari
wa mbele kushoto Inside left. Baadhi ya waanzilishi wa timu hiyo ni
Bwana Malingumu, Shaaban Feruzi, Saad Shoka, Masoud Thani na Mzee wa
Shangani.
Mara tu baada ya kujiunga na timu hiyo, Karume alichaguliwa kuwa
msaidizi nahodha. Katika mwaka 1920 Abeid Amani Karume alikubaliwa kuwa
baharia katika meli iliyoitwa Golden Crown (Taji la Dhahabu). Meli hiyo
ilichukua abiria na mizigo kati ya bandari ya Zanzibar, Dar es Salaam,
Pemba, Tanga, Mombasa na Mikindani huko Kilwa.
Baadaye alishuka katika meli hiyo na kufanya kazi katika meli
nyengine iliyoitwa Cheko. Kwa bahati mbaya, meli hiyo iligonga mwamba na
kuvunjika huko Kimbiji, nje kidogo ya Dar es Salaam lakini watu wote
walinusurika.
Kazi ya ubaharia ilimpa tija Abeid Amani Karume kwani alinunua
nyumba na viwanja kila alipopata nafasi ya kwenda nyumbani. Kwa muda
wote huo Abeid Amani Karume alifanyakazi katika meli zilizopata leseni
ya kufanyakazi katika mwambao wa Afrika Mashariki.
Katika mwaka 1922, akiwa na umri wa miaka kumi na saba, Abeid
Amani Karume alipata kazi katika meli ya kampuni ya British Indian Steam
Navigation Company ya Uingereza. Akiwa na kampuni hiyo Karume, alikaa
nje miaka mitatu hadi 1925, aliporejea nyumbani kwa mapumziko.Tayari
wakati huo, Karume alikwishatembelea nchi za
Japan,Comoro,Madagascar,China,Singapore,New Zealand,Uingereza,Marekani,
Canada,Ufaransa, Ubelgiji, India,Ureno,Hispania,Arabuni,Italia na Ugiriki.
Baada ya kupumzika kwa muda, Abeid Amani Karume alijiunga na
kampuni ya Eastern Telegraph Company na kufanya kazi katika meli ya
kampuni hiyo iitwayo Caranja. Meli hiyo ilikuwa ikitandika waya za simu
baharini kati ya Zanzibar na Aden. Aliendelea na kazi ya ubaharia hadi
mwaka 1938 alipoacha kazi hiyo kutokana na sababu mbalimbali. Karume
alishauriwa na mama yake mzazi kuacha kazi hiyo. Vilevile aliacha kazi
hiyo kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama duniani. Wakati huo,
tayari vita vikuu vya pili vya dunia vilikaribia. Baadhi ya kazi
alizofanya katika meli hizo ni Greaser, Fireman, Sailor na Headsailor.
Katika kipindi fulani cha kazi yake ya ubaharia, Abeid Amani
Karume alifanyakazi chombo kimoja na Khamis Heri Ayemba kutoka Tanga.
Wote wawili walirudi nyumbani wakati vita vya pili vya dunia
vinakaribia. Baada ya kuacha kazi hiyo,Khamis Heri Ayemba alijihusisha
na biashara huko kwao Tanga na kuwa tajiri mkubwa. Wakati wa kudai
uhuru, Ayemba alishirikiana na Peter Muhando na Mwalimu Kihere kuunda
tawi la TANU huko Tanga. Tarehe 23 Oktoba, 1955 wanachama wa mwanzo wa
TANU huko Tanga walikutana kuchagua uongozi wa chama hicho. Katika
uchaguzi huo, Khamis Heri Ayemba alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na Peter
Muhando alichaguliwa kuwa katibu.
Kutokana na kusafiri sehemu mbalimbali duniani, Abeid Amani Karume
alijifunza mengi ya kimaisha na kuona jinsi gani mataifa ya ulaya na
mabepari walivyotumia hila na ujanja kuzinyonya nchi za Afrika. Katika
safari zake za ubaharia alikumbana na matatizo kadhaa. Tatizo kubwa
zaidi alokumbana nalo ni dhoruba kali sana iliyoikumba meli yao wakati
wakitokea Australia kwenda Lorence Marques (Msumbiji).
Katika miaka ya 1930, timu za mpira wa miguu Zanzibar zilikabiliwa
na mgawanyiko. Kutokana na mgawanyiko huo, ndipo hapo mwaka 1931 timu
zote za New Kings, Vuga Boys, United Service na New Generation
zilipoungana na kuunda umoja wa michezo wa waafrika uloitwa "African
Sports Club". Timu hiyo ilikuwa na "A" na "B", ambapo Karume alikuwa
timu "A" iliyokuwa ya kwanza mwaka huo kwenda Tanganyika kucheza mechi
ya kirafiki.
Umoja huo haukwishia hapo kwani katika mwaka 1934 uliundwa umoja
wa Waafrika (African Association). Umoja huo wa Waafrika ndiyo ulogeuka
kutoka kwenye michezo na kuwa umoja wa kisiasa.
Katika mwaka 1938 bandarini Zanzibar palikuwa na vijana wa
Kiafrika walounda umoja uliyoitwa “Motorboats Association”. Vijana hao
walikuwa wakivusha abiria kutoka bandarini hadi melini kwa kutumia
mashua, kazi ambayo iliwasaidia kupata pesa chache za kuendeshea maisha.
Lakini baadaye walijitokeza wafanyabiashara wajanja wenye asili ya Asia
wenye uwezo na kununua boti za mashine na kuvusha abiria.
Wafanyabiashara hao, walitumia mbinu ya kuungana na waafrika katika
biashara hiyo.
Baada ya muda mfupi wafanyabiashara hao wenye asili ya Asia
waliunda chama chao kilichoitwa Syndicate. Taratibu wafanyabiashara hao
waliwaingiza ndugu zao na wale waafrika waanzilishi waligeuzwa vibarua
na kulipwa ujira mdogo sana. Abeid Karume aliwakusanya waafrika hao
kudai haki zao na kufanikiwa kufanya mapatano na waasia hao. Wamiliki wa
maboti hao, walikubali kuwalipa waafrika asimilia 40% ya mapato yote na
wao walichukua asilimia 60% na kugharamia uendeshaji na matengenezo ya
boti hizo.
Baada ya mafanikio hayo Abeid Amani Karume alipata sifa nyingi na
mwaka 1939 alianzisha harakati za kuunda chama cha mabaharia Zanzibar
ili kupigania haki za wafanyakazi hao. Kwa wakati huo ilikuwa vigumu
sana kuwashawishi watu wasojua mipango ya vyama vya wafanyakazi. Hivyo
basi mwishoni mwa mwaka huo wa 1939 baadhi ya wafanyakazi waloshauriwa
kuanzisha umoja huo walikataa kushiriki katika umoja huo. Karume
hakusita na juhudi zake za kuanzisha umoja huo. Mwaka huohuo wa 1939,
alionana na mzungu aitwae Bwana Douglas Basil Berber aliyekuwa Inspekta
wa polisi kuomba kibali cha kuanzisha chama cha mabaharia wa Unguja na
Pemba.
Mzungu huyo alimshauri Abeid Karume awakusanye wale wote wanaotaka
kuanzisha chama hicho na wajiunge kwa mujibu wa sheria za India.
Zanzibar kwa wakati huo haikuwa na sheria kuhusu vyama vya wafanyakazi
Waafrika.
Baada ya kuwashauri wenzake, Abeid Karume alipata watu sita
walokubali kujiunga na jumuiya hiyo. Watu hao ni Bakari Jabu, Miraji
Mselem, Juma Maalim, Ismail Mbarouk, Mbarouk Salim na Kitwana Suwedi.
Chama cha Mabaharia wa Unguja na Pemba kilipata usajili tarehe 30
Ogosti, 1949 na Makao Makuu yake yalikuwa Kisima majongoo.
Sheria ya vyama vya wafanyakazi vya Zanzibar ilipitishwa mwaka
1931. Baadaye katika mwaka 1941, sheria hiyo ilifanyiwa mabadiliko na
kuwa Sheria Nambari 3 ya vyama vya wafanyakazi.
Jumuiya za mwanzo za wafanyakazi kuanzishwa Zanzibar ni pamoja na
Jumuiya ya Mabaharia, Jumuiya ya Wachukuzi na Umoja wa Watumishi wa
Majumba ya Wazungu. Hadi kufika mwaka 1951 tayari chama cha mabaharia
kilikuwa na wanachama 83. Tarehe 26 Oktoba 1959, Abeid Karume ambaye ni
muasisi wa jumuiya ya mabaharia aliacha uongozi wa jumuiya hiyo na
kujihusisha zaidi na siasa katika chama cha ASP ,lakini aliendelea kuwa
mdhamini wa jumuiya hiyo. Kabla ya hapo katika mwaka 1942, Karume
alikuwa katibu wa African Association na Rais wa Jumuiya hiyo hapo mwaka
1953. Baadaye nafasi hiyo ilishikiliwa na Bwana Herbert Barnabas.
Kwa mara ya kwanza Sheikh Abeid Karume alifunga ndoa na Bibi Pili
binti Ahmed Ambari mwanzoni mwa miaka ya Arubaini. Mke wake wa pili ni
Bibi Ashura binti Maisara. Baada ya kutengana na wake hao wawili, Sheikh
Karume alifunga ndoa na Bibi Fatma binti Gulamhussein Ismail (Fatma
Karume) katika mwaka 1944 mwishoni mwa mwezi wa Novemba, harusi ambayo
ilifanyika huko Bumbwini Misufini.
Bibi Fatma Gulamhussein Ismail alizaliwa Bumbwini mwaka 1929 akiwa
ni mtoto wa Bwana Gulamhussein Ismail na Bibi Mwanasha Mbwana
Ramadhani. Wazazi wa Bibi Fatma Karume ni wazaliwa wa Bumbwini. Bi Fatma
Karume alipata elimu ya msingi katika skuli ya Bumbwini na kuolewa
mwaka mmoja baada ya kumaliza masomo hayo. Mara tu baada ya kufunga
ndoa, Bibi Fatma Karume na Bwana Abeid Amani Karume walihamia mtaa wa
Kisimamajongoo nyumba Nambari 18/22 mjini Unguja kwa Sheikh Karume.
Nyumba nyengine mbili za Bwana Karume zilikuwa Gongoni na Michenzani.
Bi.Fatuma Karume alijifungua mtoto wa kwanza wa kike aliyeitwa
Asha katika mwaka 1946, lakini mtoto huyo alifariki siku ya pili yake.
Mtoto wa pili wa hayati Karume ni Amani Abeid Karume aliyezaliwa tarehe 1
Novemba, 1948. Mtoto wake wa tatu ni Ali Abeid Karume aliyezaliwa
tarehe 24 Mei, 1950.
Mama yake mzazi Abeid Amani Karume, Bibi Amina binti Kadudu
alifariki dunia 1963 na kuzikwa katika makaburi ya Michenzani. Wake
wengine ambao waliolewa na Bwana Karume ni Bibi Nasra, Bibi Helemu na
Bibi Fadya ambao kila mmoja alizaa nae mtoto mmoja wa kike.
Mbali ya kuanzisha chama cha mabaharia pia Abeid Amani Karume
alikuwa muasisi wa Jumuiya ya Waafrika iliyoitwa African Dancing Club
katika mwaka 1940. Jumuiya hiyo ilikuwa na lengo la kuwaunganisha pamoja
vijana wa African Association.
Rais wa Jumuiya hiyo ya "African Dancing Club" alikuwa ni Bwana
Pearcy Baraka, Abeid Karume alikuwa Katibu Mkuu na Mweka hazina ni
Mtumwa Zaidi. Mbali ya kumiliki bendi ya muziki vilevile African Dancing
Club ilinunua banda la zamani ambalo lilibomolewa na kujengwa makao
makuu. Baadaye hapo tarehe 31 Januari, 1949 “African Dancing Club”
ilibadilishwa jina na kuitwa “African Youth Union”.
Kuundwa kwa chama cha Zanzibar Nationalist Party (Hizbu) mapema
katika miaka ya 50 na kutolewa kwa mapendekezo ya kufanyika uchaguzi
mkuu wa kwanza wa Zanzibar katika mwaka 1957 yaliwafanya viongozi wa
Jumuiya ya Waafrika African Association, na wale wa Shirazi Association
waone umuhimu wa kushirikiana. Viongozi hao waliona ulazima wa kuungana
kuwa kitu kimoja kupigania uhuru. Hivyo basi Jumuiya ya Shirazi
Association ilimtuma Bwana Haji Khatibu aliyekuwa rafiki mkubwa wa Abeid
Amani Karume apeleke shauri la kuunganishwa Jumuiya ya Waafrika na
Jumuiya ya Washirazi.
Kabla ya kukutana, kila jumuiya ilifanya kikao cha faragha
kujadili agenda ya mkutano. Shirazi Association walikubaliana
kupendekeza jina la Abeid Karume kutoka African Association kuwa Rais wa
chama kipya kitakachoundwa.
Nao African Association, walipanga kupendekeza jina la Sheikh
Ameir Tajo kutoka Shirazi Association kuwa Rais wa chama kipya
kitakachoundwa. Viongozi wa Jumuiya hizo walikubaliana kukutana kuanzia
tarehe 1 hadi 5 Februari,1957. Mkutano ulifanyika kama ulivyopangwa hapo
Mwembe Kisonge nyumbani kwa Abeid Amani Karume chini ya Mwenyekiti wake
Muhidini Ali Omar. Kwa wakati huo, nyumba hiyo ya Abeid Karume alikuwa
aliishi Hija Saleh na Haji Ali Mnoga.
Mkutano huo ulimalizika jioni ya tarehe 5 Februari, 1957 kwa
viongozi hao kukubaliana kuunganisha Shirazi Association na African
Association na kuunda chama kilichoitwa Afro - Shirazi Union.
Baadaye chama hicho kiliitwa Afro - Shirazi Party, jina ambalo
lilitolewa na Ali Khamis kutoka Shirazi Association. Viongozi 18 wa
African Association na Shirazi Association walikutana na kuunda Afro
-Shirazi Party. Kumi ni kutoka African Association na Wanane kutoka
Shirazi Association. Viongozi wa African Association walikuwa ni Abeid
Amani Karume, Ibrahim Saadala, Abdalla Kassim Hanga, Bakari Jabu, Mtoro
Rehani Kingo, Rajabu Swedi, Ali Juma Seif, Mtumwa Borafia, Saleh Juma na
Saleh Mapete. Viongozi wa Shirazi Association ni Thabit Kombo Jecha,
Muhidini Ali Omar, Ameir Tajo, Ali Khamis, Haji Khatibu, Mdungi Ussi,
Ali Ameir na Othman Sharifu.
Katika mkutano huo pia alikuwepo mgeni mwalikwa Rais wa TANU,
Mwalimu J.K. Nyerere na Katibu Mkuu wa chama cha TANU, Bwana Zubeir
Mtemvu. Pia alihudhuria Bibi Maida Springer Kemp ambaye ni Mmarekani
mweusi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Viwanda wa Marekani
American Federation of Labour Congress of Industrial Organization AFL - C
10. Bibi Springer alikuwa ziarani barani Afrika kuangalia harakati za
ukombozi na alifuatana na Mwalimu Nyerere aliyepitia Zanzibar akielekea
Tanga kuitangaza TANU.
Chama cha Afro - Shirazi Party kilimteuwa Abeid Amani Karume kuwa
Rais, Mtoro Rehani Kingo kuwa Makamo na Thabit Kombo Jecha ni Katibu
Mkuu. Wajumbe wa Halmashauri Kuu ni Ibrahim Saadala, Ali Khamis, Ameir
Tajo, Mtumwa Borafia na Muhidini Ali Omar. Baadaye wajumbe wa Shirazi
Association kutoka Pemba ambao ni Muhamed Shamte, Ali Sharif Mussa, Issa
Sharif, Suleiman Ameir na Hassan Ali waliitwa na kufahamishwa juu ya
kuunganishwa vyama hivyo.
Katika mwaka 1947 kuliundwa serikali za mitaa (Local Government)
na Baraza la Manispaa (Township Council) lilianzishwa 1954. Abeid Karume
alichaguliwa kuwa diwani (Councillor). Katika mwezi wa Juni 1957, Bwana
Karume alikwenda nchini Ghana kuhudhuria sherehe za uhuru wa taifa
hilo. Safari hiyo ilikuwa ni mwaliko wa kiongozi wa nchi hiyo, Bwana
Kwameh Nkrumah kwa vyama vyote vya kupigania uhuru barani Afrika.
Abeid Amani Karume alipendekezwa na chama cha ASP kuwa mgombea wa
kiti cha baraza la kutunga sheria wa jimbo la Ng'ambo, katika uchaguzi
mkuu wa kwanza wa Zanzibar wa 1957. Katika uchaguzi huo, Abeid Amani
Karume alijiandikisha katika jimbo la Ng'ambo kituo Nambari 84 ambacho
ni Old Shimoni School (Mao tse Tung) akiwa ni mfanyabiashara, mkaazi wa
Kisima Majongoo nyumba Nambari 18/22. Kadi yake ya kupigia kura ilikuwa
Nambari 5818. Karume alishinda kiti hicho kwa kura 3,328 dhidi ya
wapinzani wake Ali bin Muhsin Barwan wa ZNP aliyepata kura 918 na Ibuni
Saleh mgombea binafsi aliyepata kura 55.
Miaka 40 iliyopita hapo tarehe 7 Aprili, 1972 Rais wa kwanza wa
Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume aliuwawa kwa kupigwa risasi katika
jengo la Makao Makuu ya Chama cha Afro-Shirazi hapo Kisiwandui mjini
Zanzibar. Katika mfululizo wa makala haya mwandishi Ali Shaaban Juma
anaelezea historia ya maisha ya Mwanamapinduzi huyo.
Hapo tarehe 15 Januari, 1960 Abeid Karume alishtakiwa na
mfanyabiashara aitwae Punja Kara Haji mkaazi wa Darajani mjini Unguja.
Karume alishtakiwa kwa madai ya kuvunja mkataba wa kukodi bekari ya
mfanyabiashara huyo.
Kesi hiyo Nambari 4 ya 1960 (Civil Case Number 4 of 1960)
ilitayarishwa na wakili Dinshaw Karai kwa niaba ya Punja Kara Haji.
Ilidaiwa mbele ya Jaji G.J. Horsfall wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kuwa
hapo tarehe 17 Aprili,1958, Abeid Karume na Thabit Kombo waliingia
mkataba na Punja Kara Haji wa kukodi bekari ya Mchangani, nyumba nambari
2759 mali ya Punja Kara Haji.
Mkataba huo ulieleza kuwa kodi hiyo itakuwa ni ya miaka mitatu
kuanzia tarehe 1 Mei 1958 kwa malipo ya Shilingi 7,395/20. Abeid Karume
alitakiwa alipe Shilingi 550/- kila mwezi. Waraka wa makubaliano hayo
ulotayarishwa na Wakili Dinshaw Karai ulitiwa saini hapo tarehe 18
Novemba, 1959 na Punja Kara Haji kwa niaba yake na Abeid Karume kwa
niaba yake na kwa niaba ya Thabit Kombo. Mkataba huo ulishuhudiwa na
mawakili Dinshaw Karai na Hemed Said.
Akiwasilisha madai dhidi ya Karume hapo tarehe 27 Januari, 1960
Punja Kara Haji alidai kuwa tarehe 16 Novemba, 1959 Abeid Karume alifika
nyumbani kwake na kumueleza kuwa yeye na Thabit Kombo wanataka kuiacha
bekari hiyo kwa vile ilikuwa inawatia hasara.
Punja Kara Haji alieleza mahakama hiyo kuwa, baada ya kupata kauli
hiyo ya Abeid Karume walifikia makubaliano na mlalamikiwa. Abeid Karume
alitakiwa alipe Shilingi 7,395/20 kama ilivyo katika mkataba wao wa
tarehe 17 Aprili, 1958. Pia Karume alitakiwa akabidhi jengo la bekari
hiyo kwa mwenyewe hapo tarehe 31 Disemba, 1959. Akiendelea kutoa
ushahidi wake Punja Kara Haji alidai mahakamani kuwa yeye na Karume
walikubaliana fedha hizo Shilingi 7,395/20 zilipwe kwa awamu kwa
udhibitisho wa maandishi.
Awamu ya kwanza ya Shilingi 2,000/- ziwe zimelipwa ifikapo
Disemba, 1959. Fedha zilizobaki Shilingi 5,395/20 zilipwe kidogo kidogo
kwa wastani wa Shilingi 500/- kila mwezi kuanzia tarehe 1 Januari, 1960.
Fedha hizo zilitakiwa ziendelee kulipwa kwa utaratibu huo kila siku ya
mwanzo ya kila mwezi. Punja Kara alidai kuwa Abeid Karume alishindwa
kulipa Shilingi 2,000/- hapo tarehe 1 Disemba,1959 na hakulipa Shilingi
500/-ilipofika tarehe 1 Januari,1960 kama walivyokubaliana. Kutokana na
madai yake hayo, Punja Kara Haji alidai mahakamani alipwe na Abeid
Karume Shilingi 7,395/20, asilimia 9% ya riba ya mwaka kuanzia tarehe ya
hukumu na alipwe gharama za kesi hiyo.
Waraka ulomtaka Abeid Karume kufika mahakamani tarehe 8 Februari,
1960 saa 3.00 asubuhi ulitiwa saini na Mrajisi wa mahakama Hussein A.
Rahim tarehe 27 Januari, 1960.
Akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo Abeid Karume aliambia
mahakama hiyo kuwa hapo tarehe 20 Januari, 1960 alimlipa Punja Kara Haji
Shilingi 1,000/-. Pia walikubaliana kuwa deni lililobaki lilipwe kwa
wastani wa Shilingi 500/- kila mwezi. Karume alieleza kuwa licha ya
makubaliano hayo, mlalamikaji alifungua mashtaka hapo tarehe 27
Januari,1960 bila kutoa stakabadhi ya malipo ya Shilingi 1000/-
alizopewa. Baada ya kupokea waraka wa kumtaka afike mahakamani kujibu
kesi hiyo,Karume alikwenda kwa Punja Kara Haji ambaye alimweleza Karume
kuwa mashtaka dhidi yake yalifunguliwa na wakili wake aitwae Dinshaw
Karai baada ya kutofahamiana na mteja wake .
Punja alimuhakikishia Abeid Karume kuwa atamwambia wakili huyo
aifute kesi hiyo mara moja. Abeid Karume alieleza mahakama hiyo kuwa,
kwa vile aliyaamini maneno ya Punja hakuona ulazima wa kufika mahakamani
kujibu kesi hiyo. Inaelekea mlalamikaji (Punja Kara Haji) alitumia
fursa ya kutofika Karume mahakamani na kupata upendeleo wa kisheria kwa
vile kesi hiyo ilisikilizwa upande wa mlalamikaji pekee. Hivyo moja kwa
moja Punja Kara alidanganya mahakama kuwa Abeid Karume alilipa Shilingi
Elfu moja baada ya kufunguliwa mashtaka. Karume alieleza mahakama hiyo
kuwa vile vile hapo tarehe 7 Machi, 1960 alitoa mahakamani amana ya
Shilingi 2,000/- taslimu na kupatiwa stakabadhi ya malipo yenye Nambari
153/60. Lakini licha ya ukweli huo mlalamikaji aliomba mahakama hapo
tarehe 11 Machi, 1960 itoe uwamuzi wa kesi hiyo. Hata hivyo Abeid Karume
alishinda kesi hiyo na madai ya mlalamikaji yalitupiliwa mbali.
Katika mwezi wa Oktoba 1960, Sheikh Abeid Amani Karume alihudhuria
mkutano mkuu wa chama cha Malawi Congress Party huko Nkhota Kota katika
Wilaya ya kati ya Nyasaland (Malawi) akiwakilisha chama cha Afro-
Shirazi. Katika mkutano huo wanasiasa wanane wa mwisho wa Malawi
walokuwa kizuizini waliachiliwa huru. Wanasiasa hao walitiwa ndani kwa
kupinga mpango wa wakoloni wa kiingereza wa kuanzisha Shirikisho la
Rhodesia (Zimbabwe) na Nyasaland (Malawi). Baada ya kuachiliwa huru,
walikabidhiwa kwa kiongozi wa chama cha Malawi Congress Party, Dr.
Kamuzu Banda. Aliyewakabidhi wanasiasa hao kwa Dr.Banda ni Gavana wa
mwisho wa Uingereza katika koloni la Nyasaland. Msamaha huo ulitolewa
muda mfupi kabla ya nchi hiyo kupata uhuru.
Wanasiasa waloachiliwa ni pamoja na Masauko Chipembere, Matupi
Mkandawire, Chimtambi na wengineo. Mkutano huo wa chama cha Malawi
Congress Party ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Malawi. Viongozi
kadhaa wa kisiasa wa Jumuiya ya PAFMECA (Pan African Freedom Movement
for East and Central Africa) walialikwa ambapo viongozi wa ngazi ya juu
wa vyama hivyo walihudhuria mkutano huo.
Mbali ya Abeid Karume na ujumbe wake wa chama cha Afro -Shirazi
kutoka Zanzibar, pia walihudhuria Marton Malianga wa chama cha Southern
Rhodesia African National Congress cha Rhodesia (Zimbabwe)
kilichoongozwa na Joshua Nkhomo. Wengine ni Namilando Mundia wa chama
cha Zambia National Congress kilichongozwa na Kenneth Kaunda, Sheikh
Amri Abeid Kaluta na Austin Shaba wa chama cha Tanganyika African
National Union, TANU cha Tanganyika.
Vilevile alihudhuria Abdulrahman Babu na ujumbe wake wa chama cha
ZNP cha Zanzibar. Kwa lengo la kuimarisha umoja na ushirikiano kati ya
chama cha ASP na chama cha Malawi Congress Party cha Malawi, Abeid
Karume aliwaalika kuitembelea Zanzibar baadhi ya viongozi wa chama hicho
cha Malawi mapema mwaka 1965. Viongozi walotembelea Zanzibar kutoka
Malawi ni Orton Chingolo Chirwa, Yatuta Chisiza, Willie Chokani,
Augustine Bwanausi na Kanyama Chiume.
Abeid Karume alichaguliwa tena kuwa mjumbe wa baraza la kutunga
sheria katika uchaguzi wa pili wa Januari, 1961, katika jimbo la
Jang'ombe kwa tiketi ya ASP.
Mara tu baada ya kumalizika uchaguzi huo wa 1961 ulokuwa na
utatanishi Abeid Amani Karume alichaguliwa kuwa Waziri wa Afya na Mambo
ya Kienyeji katika serikali ya pamoja ya miezi sita. Uchaguzi Mkuu wa
tatu wa Zanzibar ulifanyika tarehe 1 Juni, 1963.
Karume alichaguliwa tena kuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria
katika jimbo la Kwahani na Jang'ombe. Akiwa Waziri wa Afya, Karume
alishughulikia Afya, Ajira, Ujenzi wa Nyumba, Serikali za Mitaa na
Serikali za Wilaya.
Baada ya kuundwa serikali ya Waziri Mkuu Muhammed Shamte kufuatia
uchaguzi wa 1963, Abeid Amani Karume aliteuliwa kuwa kiongozi wa
upinzani katika baraza la kutunga sheria.
Wakati wa matayarisho ya Mapinduzi ya 1964 Abeid Karume alikuwa
mwenyekiti wa kamati ya watu kumi na nne walotayarisha Mapinduzi hayo
kwa siri. Akiwa na umri wa miaka 59, Karume aliongoza Mapinduzi ya 1964
na alitangazwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi na vilevile kubaki na wadhifa wake wa Rais wa Afro- Shirazi
Party.
Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ziliungana
hapo tarehe 26 Aprili, 1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Abeid Amani Karume alichaguliwa kuwa Makamo wa kwanza wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania hapo tarehe 27 Aprili, 1964.
Akiwa Makamo wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Abeid Amani Karume aliongoza ujumbe wa watu kumi na tisa wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutembelea mikoa ya Musoma, Mwanza na
Bukoba kuanzia tarehe 5 -15 Septemba,1965. Lengo la ziara hiyo ni
kuonana na wananchi wa mikoa hiyo na kuwahamasisha kuhusu uchaguzi mkuu
wa Rais na wabunge uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa Septemba,
1965.
Mheshimiwa Karume aliteuliwa kuwa mbunge wa bunge la Tanzania
kupitia viti maalum vya kuteuliwa na Rais wa Tanzania. Karume alikuwa ni
mmoja kati ya wabunge 23 wa kuteuliwa kutoka Zanzibar kama ilivyokuwa
katiba ya wakati huo. Aliapishwa rasmi kuwa Makamo wa kwanza wa Rais wa
Tanzania katika ukumbi wa Arnatoghly mjini Dar es Salaam hapo tarehe 30
Septemba, 1965.
Katika mwezi wa Aprili 1967, Mzee Karume akifuatana na Rais wa
Tanzania Mwalimu Nyerere na wajumbe kadhaa wa serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na serikali ya Tanzania walikwenda nchini Misri kuhudhuria
mkutano wa siku nne wa nchi tano za Afrika. Mkutano huo, uliandaliwa na
Rais Jamal Abdul Nasser wa Misri. Katika ziara hiyo Mwalimu Nyerere na
Mheshimiwa Abeid Karume walitunukiwa uraia wa jiji la Alexandria. Baadhi
ya viongozi mashuhuri walotembelea Zanzibar wakati wa uhai wa Abeid
Amani Karume ni pamoja na Waziri Mkuu wa Hungary, Bwana Gyula Ka'llai,
Makamo wa Rais wa Zambia Reuben Kamanga na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Korea Bwana Kang Ryang. Wengine ni Rais Jamal Abdel
Nasser wa Misri, Rais Modibo Keite wa Mali , Rais Makarios wa Cyprus na
Rais Tito wa Yugoslavia.
Wengine ni Rais wa Hungary Bwana Pal Losonczi, Waziri Mkuu wa
Guyana Bwana Burham na Waziri Mkuu wa Swaziland, Prince Makhosini
Dlamini.
Mheshimiwa Abeid Amani Karume, kiongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar,
na mmoja wa waasisi wa Chama cha Afro-Shirazi na Makamo wa kwanza wa
Rais wa Tanzania aliuwawa akiwa na umri wa miaka 67. Mauwaji hayo
yalitokea siku ya Ijumaa ya tarehe 4 Aprili, 1972 saa 12.05 za jioni
katika jengo la Makao Makuu ya ASP Kisiwandui.
Mara tu baada ya mauaji hayo hali ya hatari ilitangazwa na msako
mkali wa wahalifu ulianza nchi nzima. Watuhumiwa kadhaa wakiwemo raia na
maofisa wa vikosi vya ulinzi na usalama walitiwa mbaroni, ambapo
mtuhumiwa mkuu akiwa ni Abdulrahman Muhammed Babu aliyekamatwa huko Dar
es Salaam.
Maziko ya Sheikh Abeid Amani Karume yalihudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa kitaifa na kutoka nchi mbalimbali duniani. Wengi wa wageni
hao walianza kumiminika Zanzibar kuanzia saa tatu za asubuhi na kwenda
kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu katika jumba la serikali
Forodhani. Baada ya kutolewa heshima za mwisho,jeneza lilitolewa nje na
kikosi cha wanajeshi ili kusaliwa katika uwanja wa Ikulu.
Baada ya marehemu kusaliwa hapo Ikulu, jeneza lilichukuliwa hadi
Makao Makuu ya ASP Kisiwandui, kupitia barabara ya hospitali ya Mnazi
Mmoja, Makumbusho, Mkunazini na kupindisha kuelekea barabara ya
Michenzani hadi Makao Makuu ya Afro-Shirazi.
Hitma ya Abeid Karume ilisomwa katika ukumbi wa klabu ya wananchi
tarehe 29 Julai, 1972 wakati wa jioni na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali pamoja na wananchi kadhaa. Kwa vile miongoni mwa malengo ya
Mapinduzi ya 1964 yalikuwa ni pamoja na kuwapatia makazi bora wananchi
wa visiwa vya Unguja na Pemba, Mzee Abeid Amani Karume aliweka jiwe la
msingi la jumba la kwanza la fleti 132 hapo Michenzani tarehe 4 Mei,
1970.
Baadhi ya taasisi ambazo zimepewa jina la Karume ni Chuo cha
Ufundi cha Mbweni Zanzibar, Kiwanja cha Ndege cha Chake Chake Pemba,
Viwanja vya mpira vya Musoma na Dar es Salaam na Kituo cha Televisheni
ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa vile miongoni mwa malengo ya Mapinduzi ya 1964 yalikuwa ni
pamoja na kuwapatia makazi bora wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba,
Mzee Abeid Amani Karume aliweka jiwe la msingi la jumba la kwanza la
fleti 132 hapo Michenzani tarehe 4 Mei, 1970. Jumba hilo la kwanza
liligharimu jumla ya Shilingi milioni 4,752,000/-. Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar ilikusudia kujenga fleti 7000 katika mji wa Zanzibar na
kutoa nafasi za makazi kwa wananchi 30 Elfu.
Kufuatia kuuwawa kwa Sheikh Abeid Amani Karume hapo tarehe 7
Aprili,1 972 watu 81 wakiwemo wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania, raia na polisi walishtakiwa kwa makosa ya uhaini katika
mahakama ya wananchi ya Zanzibar. Kesi hiyo ilianza kusikilizwa rasmi
siku ya Jumatatu tarehe 14 Mei, 1973.
Kesi hiyo Nambari 292 ya 1973 iliendeshwa na Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar, Bwana Wolfgang Dourado akisaidiwa na Ussi Khamis Haji. Katika
kesi hiyo mshtakiwa mkuu alitajwa kuwa ni Abdulrahman Muhammed Babu.
Washtakiwa tisa walikiri makosa yao, washtakiwa 54 walikana makosa
ambapo 18 akiwemo kiongozi wa njama hizo za uhaini na kutaka kuipindua
serikali halali ya ASP, Abdulrahman Muhammed Babu walishtakiwa wakiwa
hawapo kortini.
Mwanasheria Dourado aliiambia mahakama hiyo kwamba mkutano wa
mwanzo wa siri ulifanywa Dar es Salaam wakati wa sherehe za saba saba za
mwaka 1968. Babu alifanya karamu kubwa ya chakula cha mchana nyumbani
kwake, ambapo wasitakiwa kadhaa kutoka Zanzibar na Dar es Salaam
walihudhuria karamu hiyo. Siku hiyo Babu ndiye aliyetoa shauri kuwa,
kazi za wanachama wa Umma Party zipangwe vyengine na akatoa taarifa ya
dhamira ya kutaka kuipindua serikali ya ASP. Baramia aliambiwa awe ni
kiungo na mpelekaji habari baina ya Zanzibar na Dar es Salaam.
Kesi ya uhaini ilimalizika tarehe 15 Mei, 1974, ambapo washtakiwa
43 walihukumiwa adhabu ya kifo. Washtakiwa 11 walihukumiwa kwenda Chuo
cha Mafunzo miaka 15 kila mmoja na wanne walipewa adhabu ya kifungo cha
miaka 4 kila mmoja.
Washtakiwa 16 waliachiliwa kwa kukosekana ushahidi na wengine 6
walisamehewa kwa kukosa kesi ya kujibu. Mshtakiwa mmoja alifariki akiwa
kizuizini kabla ya kumalizika kesi hiyo. Ingawa washitakiwa 43
walihukumiwa adhabu ya kifo, wakiwemo tisa walokiri kupanga njama za
kumuua Sheikh Karume wote waliachiliwa huru siku ya Jumamosi ya tarehe
19 Mei, 1974.
Kwa vyovyote vile, jina la Abeid Karume halitosahaulika katika
historia ya ukombozi wa Zanzibar. Haiwezekani kuandika au kuzungumzia
ukombozi na mafanikio ya maendeleo ya Zanzibar bila kujata jina la Abeid
Karume.
(Na Ali Shaban Juma)
(Na Ali Shaban Juma)
HAYATI ABEID AMANI KARUME
Reviewed by CONVIDA FUNERAL HOME COMPANY LIMITED
on
10:17 AM
Rating:
No comments:
Post a Comment