banner image

LEO TUNATIMIZA MIAKA 23 TOKA ALIPOFARIKI MARIJANI RAJAB

ALHAMISI, Machi 23 mwaka 1995 ndio siku alipofariki  mwanamuziki gwiji mtunzi muimbaji na mpiga gitaa Marijani Rajabu. Alizikwa kesho yake Ijumaa Machi 24 kwenye makaburi ya Kisutu.
Leo hii 23 Machi 2018 familia ya gwiji huyu itafanya hitma kwa kumbukumbu ya marehemu baba yao, nyumbani kwa binti yake mkubwa huko KIjichi.
Historia ya gwiji huyu inaanzia siku alipozaliwa tarehe 3 Machi mwaka 1955, katika eneo la Kariakoo.  Mama yake alikuwa mama wa nyumbani wakati baba yake alikuwa na shughuli za uchapishaji. Maisha yake ya utoto yalikuwa ya kawaida ila alikuwa kipenda sana uimbaji wa Tabu Ley na mwimbaji mmoja wa Guinea Sorry Kandia.  Alisoma shule ya Msingi ikiambatana na elimu ya Madrasa.   Mwaka 1970 Akiwa bado shuleni, utaona umri wake ulikuwa miaka 15 tu,  alijiunga na STC Jazz, ikiwa chini ya mpiga gitaa maarufu wakati huo Raphael Sabuni, kabla ya hapo bendi hii ilikuwa unajulikana kama The Jets. Katika bendi hii Marijani aliweza kutoka nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza ambapo alikwenda Nairobi na kurekodi nyimbo zilizotoka katika label ya Phillips., hili jambo la mwanafunzi kusafiri na bendi likaleta shida na kwa vile STC ilikuwa mali ya umma akaachishwa kazi na mwaka1972 alijiunga na The Trippers ya David Mussa ambayo kwa wakati huo ilikuwa inapiga zaidi nyimbo za hoteli na za kukopi na muimbaji wao kiongozi wakati huo alikuwa Ali Rajabu. Hapa ndipo ubora wake ulifunguka haswa na kuweza kuinyanyua Trippers, ambayo sasa ilibadili jina na kuwa Safari trippers kutokana na msimamo wa serikali wakati huo wa kutaka majina ya nyumbani yatumike bala ya yale ya kigeni na  kuwa moja ya bendi maarufu za wakati huo. Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa mfululizo na kuweza kuzunguka nchi nzima. Vibao kama Rosa nenda shule, Georgina,Mkuki moyoni, viliweza kuuza zaidi ya nakala 10000 za santuri na hivyo kuwezesha bendi kuwa na vyombo vyake vizuri. Bendi wakati huo ikiwa na wanahisa wanne, ambao kwa bahati mbaya wakati bendi ndio iko juu, wakakosa kuelewana na ukawa ndio mwisho wa bendi hiyo. Marijani alishiriki kutunga, kuimba nyimbo karibu zote za Trippers sanjari na kupiga gitaa kwa baadhi ya nyimbo. Mfano wimbo Olila ambao alipiga rhythm na kuimba.
Mwaka 1976, Marijani na baadhi ya wanamuziki wa Trippers waliamua kuihama bendi na kwenda baadaye kuasisi Dar es salaam International chini ya umiliki wa Mzee Zakaria Ndabemeye ambaye bado yu hai hadi sasa. Baadhi ya wanamuziki hao ni pamoja na Abel Baltazar kutoka Msondo, Kassimu Mponda kutoka Trippers, Abdallah Gama, Joseph Mulenga, Haruna Lwali na George Kessy Omojo waliokuwa wanapiga muziki Magot pale, Said Mohamed kutoka Polisi Jazz, Cosmas Chidumule kutoka Urafiki, Belesa Kakere kutoka Biashara Jazz, Joseph Bernard kutoka Trippers, Ali Rajabu kutoka Trippers, na King Michael Enock kutoka Dar es salaam Jazz. Akiwa Dar Inter alishiriki kutunga nyimbo mbili, Betty na Sikitiko. Hata hivyo kama waswahili wanavyosema mafahari wawili hawakai zizi moja ndivyo ilivyotokea kati yake na Abel Balthazal kiasi cha hatimaye Marijani kufukuzwa ndani ya bendi kutokana na ubishi kuhusu wimbo aliotunga Marijani, kuna maelezo kuwa wimbo ulionekana unafanana na wimbo fulani toka Kongo na hivyo Marijani akatakiwa aubadilishe na ndipo ugomvi ukaanza. Hata hivyo mwishoni mwa mwaka 1978, Marijani alirejeshwa tena kundini kutokana na rundo la wanamuziki wa Dar Inter kuihama bendi kwa kishindo kikubwa na kwenda kuifungua bendi mpya kabisa ya Orchestra Mlimani Park. Aliporejeshwa Marijani alikuja na wanamuziki wengi wapya wakati huo kama akina Christopher Kasongo, Mohamed Tungwa, Mafumu Bilal, Hamis Milambo, Athuman Momba, Mzee Alex Kanyimbo na wengine na kuja na mtindo wa Super Bomboka. Katika kudhihirisha hasira zake kwa Abel, Marijani alimtungia Abel wimbo wa kumnanga ukiitwa Kidudu mtu ambao hata hivyo RTD waliukataa kuurekodi, jambo lililokuwa kawaida enzi hizo kwa redio kukataa wimbo.
 

Sifa nyingine ambayo Marijani alikuwa nayo ni kuibua wanamuziki chipukizi kama alivyofanya mwaka 1983 alipomuibua kutoka Tanga kijana Mkuu Waziri Kungugu Kitanda Milima almaaruf Fresh Jumbe ambaye kwa hakika kabisa Marijani hakujutia kumchukua kijana huyo. Alimuamini kupita maelezo kiasi kwamba wakati mwingine alikuwa akimuachia bendi aongoze na yeye anapumzika nyumbani. Mbali na Fresh, wanamuziki wengine ni kama vile Tino Masinge, Mohamed Mwinyikondo, Juma Choka na wengine kibao. Ni vizuri kuelezea hapa kuwa kadri ya maelezo yake mwenyewe marehemu  baada ya kurekodi Zuena na Mwanameka na nuimbo nyingine katika album hiyo alichoambulia ni malipo ya nauli toka RTD ya sh 2500/- tu. Kilichosikitisha zaidi ni kuwa nyimbo zao tisa ziliuzwa kwa kampuni ya Polygram bila ridhaa yao.
Hata hivyo safari ya Dar International ilikoma mwaka 1987 kutokana na sababu za kawaida za kufa kwa bendi lakini kubwa ni uchakavu wa vyombo. Hata hivyo Marijani aliendelea kufanya muziki na kwa kipindi kifupi amewahi kucheza na Kurugenzi ya Arusha na Mwenge Jazz ambayo alirekodi nayo wimbo mmoja wa Ukimwi na hata kupitia bendi ya Watafiti ambayo hatimae ilikuja kuwa 38.. Mwaka huohuo wa 1987 Marijani na Muhidin Maalim Gurumo waliliongoza kundi la wanamuziki zaidi ya 50 kutunga nyimbo maalum hasa kwa maadhimisho ya miaka 10 ya CCM na 20 ya Azimio la Arusha. Naizungumzia Tanzania All Stars. Aidha mwaka 1994 aliwahi kurekodi zong zing na marehemu Eddy Sheggy. Bendi yake ya mwisho ilikuwa ni Africulture ama Mahepe Ngoma ya Wajanja, iliyokuwa mali ya Rogers Malila, alikokuwa na wanamuziki kadhaa kama akina  Hassan Kunyata, Mgosi na wengine. Bado Marijani ataendelea kukumbukwa na wapenda muziki kote nchini na hata Afrika kwa ujumla kwa nyimbo zake zenye mafundisho na tamu huku akienzi utamaduni na ngoma za kwao Kigoma.

VIDEO YA MARIJANI AKIWA JUKWAANI
LEO TUNATIMIZA MIAKA 23 TOKA ALIPOFARIKI MARIJANI RAJAB LEO TUNATIMIZA MIAKA 23 TOKA ALIPOFARIKI MARIJANI RAJAB Reviewed by SHEDrack Mtawa on 10:10 AM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.