Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana
ulikuwa eneo la majonzi makubwa baada ya miili ya askari 14 wa Jeshi la
Wananchi (JWTZ), waliouawa na waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC), kufika nchini hatimaye.
Miili
hiyo ilirejeshwa majira ya jioni na kupokelewa na umati wa askari wa
JWTZ wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk.
Hussein Mwinyi pamoja na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo.
Ni
mara ya kwanza kwa wanajeshi wengi kiasi hicho wa JWTZ kuuawa katika
misheni ya kulinda amani, kwa mujibu wa Jenerali Mabeyo aliyekuwa
akijibu maswali ya waandishi wa habari uwanjani hapo.
Miili hiyo ililetwa na ndege maalum ya Umoja wa Mataifa huku ikiwa imefunikwa bendera ya UN.
Baada
ya kuwasili, kwa huzuni wanajeshi walianza kuchukua mwili mmoja baada
ya mwingine na kuhamishia katika magari maalum yaliyokuwa yameandaliwa.
Kila
mwili ulibebwa na wanajeshi nane wakati wa kuhamishia katika magari
hayo kwa ajili ya kusafirisha kwenda kuilaza katika Hospitali Kuu ya
Jeshi ya Lugalo, jijini.
Jumla ya magari saba yalitumika kubebea miili hiyo, kila moja ikibeba miili miwili na kusindikizwa na kundi la wanajeshi.
Akizungumza
kabla ya kuanza safari hiyo ya kwenda Hospitali ya Lugalo, Dk. Mwinyi
alisema miili hiyo inatarajiwa kuagwa Alhamisi katika viwanja vya Wizara
ya Ulinzi, eneo la Upanga.
Pia
alisema tukio la kuuawa kwa wanajeshi hao wamelipokea kwa masikitiko
makubwa na kwamba wataendelea kuchukua tahadhari ili kuzuia kutokea kwa
tukio kama hilo tena.
Kwa upande wake, Jenerali Mabeyo alisema tukio kama hilo ni la kwanza kutokea na kwamba hawajatetereka.
“Unavyolinda
amani, lazima utegemee lolote, na tukio hili ni la kwanza katika
kipindi cha miaka mitano," alisema Jenerali Mabeyo. "Hatuna hofu."
"Isipokuwa unaposhambuliwa, unajitazama umekosea wapi halafu unajirekebisha."
Aidha,
mkuu wa majeshi alisema hali ya wanajeshi waliojeruhiwa ambao wako
Kinshansa, DRC na nchini Uganda inaendelea vizuri na kwamba mmoja
aliyepotea kati ya wawili amepatikana.
Kufuatia
vifo hivyo, Rais John Magufuli ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu alituma
salamu za rambirambi kwa Waziri Mwinyi, Jenerali Mabeyo, maofisa wote wa
Jeshi na kwa familia zote za marehemu mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika
salamu hizo Rais Magufuli alisema: “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa
taarifa za kuuawa askari wetu kumi na wanne na wengine arobaini na wanne
kujeruhiwa, na wawili hawajapatikana huko DRC wakati wakitekeleza
majukumu ya ulinzi wa amani.
"Natoa
pole sana kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na familia, (na)
wakati tukisubiri taarifa kamili kutoka DRC niwaombe Watanzania tuwe na
subira."Mungu wetu yuko pamoja nasi."
Taarifa
ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres
Ijumaa ilisema shambulio hilo ndilo baya zaidi kuwahi kutekelezwa dhidi
ya walinda amani wa umoja huo katika historia yake miaka ya karibuni.Pia
alielezea kusikitishwa na tukio hilo.
“Ningependa
kueleza kusikitishwa kwangu na shambulio hilo lililotekelezwa usiku wa
jana (Alhamisi) dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini DRC,"
alisema katika taarifa hiyo.
"Shambulio
hilo lilitekelezwa kwenye kambi ya jeshi ya Semuliki, eneo la Beni
katika mkoa wa Kivu Kaskazini.Taarifa ya UN ilisema pia wanajeshi watano
wa Jeshi la DRC (FARDC) waliuawa kwenye shambulio hilo.
Majonzi miili 14 ya Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ikipokelewa
Reviewed by CONVIDA FUNERAL HOME COMPANY LIMITED
on
9:30 PM
Rating:
No comments:
Post a Comment