banner image

Kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu kifo cha SAMUEL SITTA

Name: Samuel John Sitta
Born: December 18, 1942, Urambo District
Died: November 7, 2016, Munich, Germany
Education: University of Dar es Salaam
Party: Chama Cha Mapinduzi
Spouse(s): Margaret Sitta
Resting place: Urambo District, Tanzania
Historia ya samuel sitta 1942-2016
  • Atakumbukwa zaidi kwa uongozi wake katika Bunge la tisa
  • Bunge Maalum la Katiba
  • Mgomo wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa mwaka 1966 


Samuel John Sitta alizaliwa Desemba 18, 1942 huko wilayani Urambo Mkoa wa Tabora. Sitta alisoma Shule ya Msingi Urambo kati ya mwaka 1950 – 1953, kisha alikwenda Wilaya ya Sikonge mwaka 1954 – 1957 na kuendelea na masomo ya “Middle School” katika shule ya “Sikonge Middle School”. Baadaye mwaka 1958 – 1963 alianza masomo ya sekondari Shule ya Wavulana Tabora yaani “Tabora Boys” kidato cha I – IV na cha V – VI.Mara tu baada ya kuhitimu masomo ya sekondari, Sitta alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea Shahada ya Sheria (LLB) mwaka 1964 na kuhitimu mwaka 1971.
Sitta amesoma shahada yake kwa miaka 7 kwa sababu mwaka 1966, wakati yuko mwaka wa pili na akiwa kiongozi wa wanafunzi UDSM, wanafunzi waligoma na kuandamana kupinga kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kukatwa mishahara yao baada ya JKT. Hoja ya wanafunzi ilikuwa na mantiki kubwa, kwamba mbona vigogo wa serikali na wanasiasa wanalipwa mishahara minono na marupurupu makubwa? Baada ya shinikizo hilo la wanafunzi Mwalimu Julius Nyerere alikubali kupunguza mshahara wake wa Sh4,000 bila kodi akaagiza pia mishahara ya mawaziri ipunguzwe kwa asilimia mbili. Miezi miwili baadaye akatangaza Azimio la Arusha (Februari 5, 1967) kuyapa uzito malalamiko ya wanafunzi hao. Watukutu wawili – Sitta na Wilfred Mwabulambo (sasa marehemu) na wengine kadhaa – waliojitia wazimu na kutetea kile walichokiita haki zao, (haki za wakulima na wafanyakazi), walimshutumu Mwalimu Nyerere kwa maneno makali wakidai “…ni heri wakati wa ukoloni kuliko utawala wa Mwalimu”.
Mwalimu Nyerere alikasirika na kuwafukuza chuo wanafunzi wote 400 kwa kile alichokiita “kwenda kufunzwa adabu majumbani mwao”. Miezi kumi baadaye, baada ya Nyerere kushawishiwa na hasira kutulia akaamua kuwarudisha chuoni wanafunzi 392. Viongozi wa mgomo; Sitta na wenzake 7 walitiliwa ngumu, hawakurejeshwa chuoni.

 Busara za viongozi wa chuo zilifanya Mwalimu aliliwe zaidi na kuandikiwa barua mbili maalumu na chuo zenye Kumb. Na. C3/Sa.13 ya 2/3/1967 na C3/Ss.13 ya 9/07/1967. Mwalimu alikubali kilio hicho na kuwaruhusu vijana hao wanane warudi kwa sharti kwamba wale watukutu wawili (Sitta na Mwabulambo) watandikwe viboko na “Mwalimu Nyerere” mwenyewe. Hii ndiyo ilikuwa pona ya Sitta ambaye alirejea UDSM na kuendelea na masomo kwa miaka kadhaa hadi alipohitimu mwaka 1971.Wakati Sitta anarudi chuoni tayari alikuwa mwajiriwa wa Kampuni ya Mafuta ya “CALTEX OIL” kama Meneja wa Tawi (1967 – 1969) na mwaka 1969 – 1975 aliajiriwa na Shirika la Maendeleo la Taifa kama Katibu na Mkurugenzi wa Utawala.Baadaye mwaka 1976 Sitta aliamua kujiendeleza kielimu katika masuala ya Usimamizi nchini Uswisi kwenye Chuo Kikuu cha IMEDE ambako alihitimu Stashahada ya Juu ya Usimamizi mwaka huohuo 1976.
Chini ya mfumo wa chama kimoja, Sitta amekuwa kiongozi wa juu wa CCM na serikali akiwa mbunge, mkuu wa mkoa na waziri katika nyakati tofauti na ameendelea kuwa mbunge na waziri katika mfumo wa vyama vingi.
Mbio za ubungeEnzi za chama kimoja 1975 – 1995 Sitta amekuwa mbunge wa Jimbo la Urambo (kabla halijagawanywa na kuwa Urambo Magharibi na Mashariki) na pia alifanikiwa kuwa waziri kwa nyakati tofauti. Kwa mfano wakati wa kipindi cha mwisho cha Mzee Mwinyi, Sitta alikuwa Waziri za Katiba na Sheria.
Mwaka 1995 Sitta aliingia kwenye mapambano mapya ya siasa za vyama vingi na kwa bahati mbaya akawa mmoja wa vigogo walioangushwa na wabunge wa NCCR. Mshindani wake mkuu alikuwa Msina Jacob Abraham. Msina alishinda kwa kura 10,788 dhidi ya 9,497 za Sitta. Sitta alirudi tena kwenye jukwaa la siasa mwaka 2005 kwenye uchaguzi mkuu na aliwashinda wapinzani wake wakuu Lumatiliza Yotamu Lubungila wa NCCR na Wilson George Ntakamulenga wa CUF. Sitta alipata kura 28,660 (72.3%) na kurejesha heshima yake jimboni Urambo Mashariki. Kurudi kwa nguvu kulimpa nafasi ya kuwania na kuteuliwa na CCM kugombea uspika wa Bunge la Tanzania na akaliongoza Bunge la Tisa kwa mafanikio na changamoto nyingi. Mwaka 2010 Sitta alishiriki tena uchaguzi Urambo Mashariki akawashinda wapinzani wake wakuu Msafiri Abdulrahmani Mtemelwa (Chadema) na Zombwe Lotto Edward (CUF) kwa kupata kura 19,947 (70.47%). Baada ya ushindi huo, Sitta alijaribu tena kuwania uspika bila mafanikio; Sitta akapoteza ndoto za uspika na ukahamia kwa mwanamama Anne Makinda. Rais Jakaya Kikwete alipotangaza Baraza la Mawaziri mwaka 2010 alimpa Sitta Wizara ya Afrika Mashariki kama Waziri, wadhifa aliodumu nao hadi mwanzoni mwa mwaka 2015 alipobadilishwa na kupelekwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.
Mwaka 2014 wakati wa Bunge maalum la katiba Samuel Sitta alichaguliwa na kufanikiwa kuliongoza Bunge Maalum la Katiba.
Kuelekea Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Samuel Sitta alichukua fomu katika chama chake cha CCM ili kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini hakufanikiwa kupata ridhaa ya Chama chake kuwa mgombea wa Urais.


‘THATS life’ ni neno la mwisho la Spika mstaafu Samuel Sitta baada ya kuambiwa na daktari wake ambaye alikuwa anamtibu nchini Ujerumani kuwa asingeweza kupona kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.
Kauli hiyo ilitolewa na Benjamin alipozungumza na waandishi wa habari nyumbani kwao Masaki, Dar es Salaam jana, akimnukuu marehemu baba yake.
Alisema mpendwa baba yake alikuwa amekwisha kujiandaa kwa kifo baada ya daktari wake kumwambia hivyo, jambo ambalo lilimfanya kufa kifo chema.
“Daktari aliyekuwa anamtibu alimwambia baba kuwa hawezi kupona, lakini alimjibu ‘that’s life’ na hakuendelea tena,” alisema.
Alisema katika kipindi cha uhai wake baba yake alishika nyadhifa mbalimbali, jambo lililomjengea umaarufu ndani na nje ya nchi.

Benjamin alisema Mzee Sitta alisimamia mambo mbalimbali yakiwamo haki na pale alipoamua kutetea jambo lake.
Alisema katika kipindi hiki cha msiba, familia imefarijika baada ya kuona kila mmoja anamzungumzia jinsi anavyomfahamu.
“Kila mmoja anasema lake katika kipindi hiki cha msiba, hii inaonyesha jinsi gani watu wanamvyomfahamu kutokana na misimamo yake anapoamua jambo lake liende,” alisema.
Alisema kuwa familia inamshukuru Rais Dk. John Magufuli na Ofisi ya Bunge kwa jinsi walivyokuwa karibu nao tangu anaumwa hadi kifo chake.
Benjamin alisema kuwa taarifa za msiba zilipowafikia, Rais Magufuli aliwasiliana nao na kuwapa pole, jambo ambalo liliwafariji.


Kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu kifo cha SAMUEL SITTA Kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu kifo cha SAMUEL SITTA Reviewed by CONVIDA FUNERAL HOME COMPANY LIMITED on 1:32 PM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.