banner image

MWILI WA NGULI WA MSONDO NGOMA, SHABANI DEDE KUZIKWA KISUTU LEO

Mwili wa nguli wa Muziki wa Dansi Tanzania aliyekuwa akiitumikia Bendi ya Msondo Ngoma, Shaban Dede, unatarajiwa kuzikwa leo Ijumaa katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Mbali na kuitumikia Msondo Ngoma, pia Dede aliwahi kupita bendi kadhaa zikiwemo DDC Mlimani Park, Bima Lee na Ochestra.
Dede amefariki dunia jana asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa amelazwa katika jengo la Mwaisela wadi namba tano kwa zaidi ya wiki mbili akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.
Mtoto wa marehemu, Hamad Dede amesema baba yake alifikwa na umauti huo jana majira ya saa mbili asubuhi, baada ya kusumbuliwa kwa muda na tatizo la ugonjwa wa kisukari.
“Kwa ufupi tu nikwambie msiba utakuwa Kariakoo Mtaa wa Congo na maziko yatafanyika kesho (leo) saa 7:00 mchana kwenye Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam,” alisema.
Kwa upande wa meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti, alisema: “Tumesikitishwa sana na msiba wa mmoja wa watu muhimu ndani ya bendi yetu, japo hatuna jinsi, nakumbuka Dede tulifanya naye kazi mara ya mwisho mwezi wa sita kabla ya mfungo wa Ramadhani ambapo tulikuwa na tamasha la pamoja na bendi ya Sikinde na alifanikiwa kuimba wimbo mmoja tu akashindwa kuendelea kufuatia hali yake kusumbuliwa na ugonjwa huo.”
MWILI WA NGULI WA MSONDO NGOMA, SHABANI DEDE KUZIKWA KISUTU LEO MWILI WA NGULI WA MSONDO NGOMA, SHABANI DEDE KUZIKWA KISUTU LEO Reviewed by CONVIDA FUNERAL HOME COMPANY LIMITED on 8:30 PM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.