banner image

KWAME NKRUMAH DAY (27-APRIL)

Born: September 21, 1909, Nkroful, Ghana
Died: April 27, 1972, Bucharest, Romania
Kwame Nkrumah na mke wake na machifu huko Ghana siku ya Januari 20, 1963
Kama inavyokumbukwa, Kwame alizaliwa katika kijiji cha Nkroful, magharibi mwa Ghana, Septemba 21, 1909.
Maisha ya Kwame tangu kuzaliwa kwake hadi alipofariki Aprili, 1972 akiwa na umri wa miaka 63 tu, yanajulikana sana. Alikuwa msomi na mwanaharakati aliyepigania na kuongoza harakati za kudai uhuru, ukombozi na Umoja Afrika.
Alitetea kwa nguvu na akili zake zote, heshima na haki ya Afrika na watu Weusi duniani kote. Na zaidi ya yote, alikuwa katika mstari wa mbele kupinga ubeberu, ukoloni na ukoloni mamboleo.
Kwame Nkrumah hakuwa kiongozi wa kawaida. Alikuwa 'nabii' mwenye ujumbe maalumu kwa Afrika na watu Weusi duniani. Na kama ilivyo ada: Nabii kwa nadra hukubalika kwao. Alikumbana na vikwazo vingi lakini hatimaye akapata ushindi mkubwa.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) mwaka 2000, baada ya kuwahoji wasikilizaji wake wengi, lilimtangaza kuwa ni "Mtu Mashuhuri wa Milenia".
Kwa wale wanaomfahamu Kwame, huo ndio ukweli wenyewe. Kwa Afrika yetu, hakuna kiongozi wa mfano wake, labda wawili watatu hivi ambao wengi tunawaelewa. Na itakuwa hivyo kwa miaka hata 100 ijayo.
Baada ya kuishi Marekani kwa miaka 10, Kwame alikwenda Uingereza kwa masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha London.
Siku moja akiwa dukani kununua kitu, mtoto wa mwenye duka akasema kwa mshangao: 'Mama, kijitu hiki kinaongea?" Yule mtoto hakuamini kwamba mtu Mweusi ni mtu kama yeye, na kwamba anaweza kuongea Kiingereza!
Mwenye duka, kwa uungwana wake, alimwomba radhi Kwame. Lakini huyo kijana hakukosea katu. Historia ya Afrika ya Waafrika na watu Weusi duniani na kwa miaka mingi, imekuwa ni ya kuonewa, kunyanyaswa na kudharauliwa.
Hata zama hizi, hali haijabadilika sana. Bado safari yetu ya ukombozi ni ndefu tu. Ni kweli tumepiga hatua hapa na pale lakini, Afrika na Waafrika- mbele ya mataifa mengine duniani tungali wanyonge na watu wa kuchezewa!

Kwame atakumbukwa kwa kupigania uhuru wa Ghana iliyokuwa nchi ya kwanza kusini mwa Sahara kujinyakulia uhuru kutoka kwa Waingereza Machi 6, 1957.
Aliporejea nchini humo mwaka 1947, alijitumbukiza katika harakati za kudai uhuru. Kwanza kama Katibu Mkuu wa Chama cha United Gold Coast Convention na baadaye kama kiongozi mkuu wa Convention Peoples Party (CPP).
Alibadili mustakabali wa siasa za Ghana na Afrika. Alijenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa watu wake –vijana, wakulima, wanawake, wamachinga, wasomi, wafanyakazi na wafanyabiashara mpaka wakoloni wakaona hawana pa kupita.
Mabadiliko ya katiba yakafanyika mwaka 1951, na mwaka uliofuata Kwame akachaguliwa kutoka jela kuwa Waziri Mkuu. Miaka sita baadaye, Ghana ikawa huru.
Kwame alitamka dhahiri ya kuwa uhuru wa Ghana haujakamilika endapo nchi moja ya Bara la Afrika itaendeela kubaki chini ya ukoloni. Na tangu wakati huo, Ghana ikawa kitovu cha harakati za uhuru na ukombozi wa nchi nyingine za Afrika.


Ghana ilitoa mchango wa hali na mali kwa wapigania uhuru wote Afrika. Kwame akabeba jukumu la kuisemea na kuitetea Afrika nzima. Matokeo yake yanaeleweka. Mwaka 1957, zilikuwapo nchi nane huru za Afrika. Ilipofika mwaka 1963, nchi zaidi ya 35 zilikwsha kupata uhuru.
Labda kazi kubwa kuliko yote aliyoifanya ni harakati za kujenga na kuendeleza Umoja wa Afrika. Mwaka 1958, aliitisha mkutano wa tatu wa Afrika (All Africa Peoples Conference) mjini Accra.
Aliwahimiza wenzake kuharakisha ukombozi wa Afrika yote, na kuwataka kujikita katika ujenzi wa Umoja wa nchi za Afrika United States of Africa (USA) kwa kuzingatia mwenendo wa historia ya dunia, na kwa kuzingatia nafasi ya Waafrika na watu Weusi katika historia yao.
Aliamini kabisa ya kuwa heshima na utu wetu vitapatikana pale tu Afrika nzima itakapokuwa huru, pale itakapokuwa imeungana kama taifa na kuwa nchi moja kubwa.
Msimamo wake huo na imani yake hiyo vikawa ni ajenda yake ya wakati wote. Maisha yake yote, kazi zake zote, na fikra zake zote zikawa zimeelekezwa katika kushughulikia mambo hayo.
Mwaka 1963, nchi za Afrika zilianzisha Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), na makao Makuu yakawa Addis Ababa, Ethiopia. Kwame alikuwa mwanzilishi na hiyo ilikuwa ni hatua njema.
Ila Kwame aliwaomba wenzake waunde si tu chombo hicho bali taifa kubwa na jipya la Afrika lenye Serikali Kuu ya Afrika, Jeshi la Afrika na taasisi nyinginezo za kidola. Alitaka umoja wa Afrika papo kwa hapo. Wenzake walimkatalia.

Wengi wao na hasa Mwalimu Julius Nyerere, alieleza ya kuwa japo Afrika nzima lazima iungane lakini umoja unatakiwa kujengwa, na kwamba hautakuja kama miujiza.
Tofauti hizo mpaka leo zipo. Lakini azma na lengo la kuwa na taifa kubwa lililoungana la Afrika bado viko palepale. Na ukweli huo umethibitishwa na hatua zilizochukuliwa na viongozi wetu wa sasa za kuimarisha Umoja wa Afrika kwa kuanzishwa umoja mpya wa AU na taasisi zake mpya. Aliyekuwa kiongozi Mkuu wa Libya, kanali Gadhafi alikuwa kinara wa juhudi hizi mpya ambazo ipo siku zitazaa matunda.
Kwake Nkrumah alikuwa kiongozi makini na hodari. Kwa watu wa kawaida, alikuwa ni mwenzao. Hakuwa na makuu na wala kuwa na tamaa ya mali. Maisha yake yote aliishi kutumikia watu.
Leo watu wa Ghana wanamkumbuka na kumuenzi kwa juhudi zake za kujenga taifa lenye usawa, haki na heshima kwa watu wote. Alichukia sana dhuluma na unyonyaji. Alichukia sana ubwanyenye na ufahari.
Alipenda viongozi wenzake wawe karibu na watu, wawasikilize, waishi nao, wajifunze kutoka kwao na muda wote wawe karibu nao.
Alifundisha ya kuwa viongozi na wananchi ni mithili ya samaki na maji, wote wanategemeana. Matumaini yetu ni kwamba viongozi wetu wa sasa wataiga mfano wake.
Nakumbuka mnamo mwaka 1960, nilimwuliza mwalimu wangu kuhusu kitanda cha dhahabu kinafafanaje. Akaniuliza nimepata wapi habari hizo.
Nikamweleza kuwa nilisoma kwenye gazeti la TANU la Mwafrika kwamba waziri mmoja wa Ghana, Krubo Edusei alimnunulia mke wake kitanda hicho kutoka Uingereza.
Mwalimu wangu akawaeleza walimu wenzake na nikaitwa kwenye chumba cha walimu kuhojiwa. Siku ya pili nikawaletea nakala ya gazeti hilo. Waziri huyo aliachishwa uongozi mara moja na Kwame.
Pamoja na Kwame kujitahidi kujenga taifa huru lenye usawa, haki, heshima na umoja, bado alipambana na viongozi mafisadi ambao walitawaliwa na tamaa za mali na anasa.
Na hii si ajabu maana ndivyo yalivyo maumbile yetu binadamu. Alichofanya Kwame ni kuwabana viongozi wake na watendaji wake kwa kuanzisha mfumo wa maadili ya uongozi.
Viongozi walizuiwa kujiingiza kwenye biashara na shughuli za kujikusanyia mali. Walitakiwa kuishi maisha ya kawaida na kutumikia umma. Wale walioshindwa waliombwa kujiishia maisha yao ya kuchuma na kuhodhi ukwasi.
Na hawakuwa wachache. Mmoja wao alikuwa Komla Gdemah aliwahi kusema: "Kuwa mjamaa haina maana utupe au kugawa mali zako ulizohodhi."
Kwa Afrika ya leo, tuna mambo ya msingi ya kujifunza kutoka kwa Kwame, na hasa viongozi wetu wa sasa na kesho. Tukumbuke kwamba hatumpati tena Kwame na watu wa aina yake. Itakuwa ajabu ya karne hilo kutokea.
Lakini tumeachiwa urithi mkubwa nao. Jambo muhimu ni kutambua na kuzingatia historia ya bara letu na watu wake.
Ni utambuzi na mzingatio huo ambavyo vitatuwezesha kupanga na kuendeleza mustakabali wa maisha yetu. Kama Azimio la Arusha lilivyobaini: "Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumedharauliwa kiasi cha kutosha na tumenyonywa kiasi cha kutosha."
Leo na miaka 100 ijayo, hali ya Afrika na Waafrika itaendelea kuwa hivyo. Adui mkubwa wetu atabaki kuwa yule yule: Ubeberu na Ukoloni Mamboleo! Waafrika tusidanganyike. Bado sisi na nchi zetu tu wanyonge wa kupindukia.
Pamoja na juhudi zetu za kujiletea maendeleo, mazingira ya ubeberu na Ukoloni Mamboleo, bado ni yale yale na kwa kweli yanazidi kujitanua. Hatuna kauli duniani, hatuna sauti wala nguvu kwenye taasisi za kimataifa.
Ni wasindikizaji na wasikilizaji. Mathalani, kwenye taasisi za kifedha kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, nani anatusikiliza? Mambo yetu mengi tunayafanya kwa kuelekezwa na wakubwa wa dunia hii kuanzia siasa, uchumi, utamaduni na mengineyo.
Sisemi tusiyafanye. Lakini tufanye tukijua kwamba sisi ni matishari; wenye mali na manowari wapo! Sisi ni wa kuvutwa tu, bendera fuata upepo! Huo ndio ubeberu na Ukoloni-Mamboleo.
Kwame alielewa hivyo na ndiyo maana akahimiza tujenge, mara moja ikiwezekana taifa moja kubwa la Afrika. Umoja ni nguvu. Mataifa 53 ya Afrika ni kielelezo cha unyonge wetu. Tungelikuwa sisi ni nchi moja kubwa, mustakabali wetu duniani ungekuwa mwingine.
Hata pamoja na umasikini wetu, bado hadhi na heshima yetu vingelikuwa juu. Maana tembo si sawa na sungura! Kweli wote ni wanyama. Lakini mmoja mkubwa na mwingine ni mdogo.
Leo mataifa yenye heshima ni mataifa makubwa – Marekani, Urusi, China, India, Brazil n.k. Nchi za Ulaya leo zinahangaika kuimarisha umoja miongoni mwao kwa lengo la kuwa na taifa kubwa la Ulaya.
Waafrika lazima tuige mifano hiyo. Ujenzi wa taifa kubwa la Afrika haukwepeki. Tunachelewa, lakini ipo siku tutafika.
Utajiri na rasilimali zetu havina budi kutumika kwa manufaa na faida ya bara letu kwanza. Umoja wetu ndiyo kinga yetu pekee.
Na kwenye muktadha huo, ni vyema tuendeleze juhudi za kuyajenga mataifa yetu madogo kwa kuzingatia misingi ya umoja ya uhuru, heshima, usawa na haki. Historia ya nchi za Afrika miaka 50 iliyopita si nzuri sana.
Tumeuana vya kutosha sisi kwa sisi. Tumeonewa na serikali zetu wenyewe na za nje. Tumejenga tawala za kiimla na kifashisti. Kwa ujumla, ni wachache wetu tunaoweza kusema tumefaidi matunda ya uhuru.
Umasikini, ujinga, maradhi na ufisadi vinatamalaki sehemu kubwa ya bara letu. Hali hii isiruhusiwe kuota mizizi. Tuendeleze juhudi zetu za kupanua uhuru wa watu wetu.
Tupanue elimu na tuimarishe uchumi kwa kujenga uchumi unaokidhi mahitaji ya msingi na ya lazima ya watu wetu. Tuimarishe huduma za jamii kwa watu wetu.
Na kwa kuwa watu wetu wengi wanaishi vijijini, tuwekeze na kuimarisha kilimo chetu kiwe cha kisasa na cha kutosheleza mahitaji yetu ya chakula na biashara. Rasilimali zetu kama madini, utalii n.k zitumike kutuinua sisi na nchi zetu badala ya nchi za nje.
Ili yote yafanikiwe, tunahitaji viongozi kama kina Kwame Nkrumah wengine wengi. Uongozi bora, wenye msimamo, usioyumbayumba na usiokuwa wa utumwa wa mali na tamaa za umamluki ni muhimu.
Mwaka 1966, Jeshi la Ghana kwa maelekezo ya Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), liliangusha Serikali ya Ghana, na Kwame akaenda uhamishoni Guinea.
Walieneza propaganda kali kwamba Kwame alikuwa fisadi na mhujumu wa fedha na mali za Ghana. Lakini baadaye ikadhihirika ya kuwa huo ulikuwa ni uongo wa mchana.
Kwame alikuwa ni kiongozi masikini. Hakuunda, yeye na mkewe Fatma, kitu kinachoitwa FATKWA (Fatma-Kwame) ili kukusanya mali binafsi. Kamwe hakuficha fedha Uswisi.
Mpaka leo, watoto wake wanaishi kama sisi wengine. Uongozi unaohitajiwa katika Afrika ya sasa ni ule unaoheshimu watu wetu wote, na katika hali zao zilivyo.
Nchi zetu, baada ya miaka 50 ya uhuru, zimekua. Ni kweli hazijakomaa, lakini zimekua. Watu wetu ni weledi zaidi, si wajinga kama zamani. Hii ni nguvu mpya.
Viongozi wetu lazima waheshimu na kuthamini mazingira haya mapya. Kuna maua takriban 1,000 yamechanua. Zipo fikra, hoja na dhana kadha wa kadha katika jamii zetu. Zizingatiwe. Zisibezwe wala kupuuzwa.
Kama alivyowahi kufafanua Kwame, bara la Afrika ni 'pilau' yenye viungo vingi, hususan vya kutoka ndani ya Afrika yenyewe, Mashariki ya Kati na Mbali na Ulaya.
Siku hizi katika nchi zetu, tunajenga demokrasia ya vyama vingi. Tunazo pia taasisi za kiraia. Na bila shaka tunao raia mmoja mmoja. Hatuna budi kuimarisha mshikamano wa makundi haya yote, maana nchi zetu ni zetu wote kwa pamoja.
Hayupo mwenye hadhi kuliko mwingine. Na Afrika yetu ni yetu wote. -Waswahili, Wapagani, Waislamu, Wakristo, Wahaya na Wamatumbi. Hakuna wenye ukiritimba au hatimiliki ya fikra na uongozi.
Kwame Nkrumah alitoa mchango wake mkubwa kupigania uhuru, umoja na ukombozi wa Afrika na watu Weusi. Kazi na juhudi zake zitakumbukwa daima. Wajibu wetu, na hasa kizazi kipya cha vijana wa Afrika, ni kuendeleza pale alipoishia.
Afrika bado ina changamoto za kutosha kwa yeyote ambaye yupo tayari kuitumikia kwa namna yoyote ile.
Tunapoadhimisha karne moja ya Osagyefo Kwame Nkrumah, tukumbuke muda wote kwamba bado ni" Aluta continua! Mungu Ibariki Afrika!
KWAME NKRUMAH DAY (27-APRIL) KWAME NKRUMAH DAY (27-APRIL) Reviewed by CONVIDA FUNERAL HOME COMPANY LIMITED on 5:00 PM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.