banner image

MIAKA 36 BAADA YA KIFO CHAKE MFALME WA MZIKI WA REGGAE (BOB MARLEY)

Robert Nesta Marley, ambaye anafahamika zaidi kama Bob Marley, na hii inatokana na kuwa Bob ni kifupi cha Robert, alizaliwa tarehe 6 Februari, 1945 kwenye shamba la babu yake ambaye alikuwa mzazi wa mama yake katika kijiji cha Nine Mile , Saint Ann Parish Jamaica. Baba yake aliitwa Notval Sinclair Marley na mama yake aliitwa Cedella Booker. Bob alipewa jina la Nesta Robert Marley, lakini wakati wa kuandikwa passport yake jina la kati likabadilishwa na hivyo wengi tunamfahamu kama Robert Nesta Marley. Bob akiwa na umri wa miaka 10 baba yake akafariki kwa ugonjwa wa moyo, hiyo ilikuwa mwaka 1955. Hivyo Bob alilelewa na mama yake, ambaye hata kabla cha kifo cha mumewe alikuwa peke yake kutokana na mume wake kuwa safarini muda mwingi. Bob alianza shule ya msingi hapohapo Nine Mile, na kati ya marafiki zake wa utotoni alikuwa Neville Livingston ambaye hujulikana zaidi kwa jina la Bunny Wailer, walianza kujifunza muziki pamoja wakati wakiwa shule ya msingi ya Stepney na kuendelea walipoingia sekondari. Alipokuwa na umri wa miaka 12, Bob na mama yake wakahamia Trenchtown, katika jiji la Kingston. Mama yake Bob Marley akazaa na baba yake Bunny Wailer, mzee Thadeus Livingston, binti aliyeitwa Pearl, na hivyo huyo binti kuwa ni mdogo wake wa Bunny Wailer na mdogo wake Bob Marley. Kwa hiyo sasa Bob na Bunny wakawa ndugu haswa na wakawa wanaishi nyumba moja na mapenzi yao kwenye muziki yakazidi wakawa wanasikiliza na kujaribu kupiga muziki waliokuwa wakiusikiliza kwenye radio na pia Jamaica ikawa na muziki mpya uliokuwa umegunduliwa huko ukiitwa Sca music.
Muda is mrefu wakaanza kujiunga na vya muziki vya muziki vya Kingston, na huko walikutana akina Peter Tosh, Beverley Kelso na Junior Braithwaite, ambao wote walikuja kutingisha dunia katika muziki wa reggae. Wakati huo Bob na Bunny walipendelea zaidi kuimba, lakini pia Bob akawa anafundishwa kupiga gitaa, msingi uliomfanya kuja kutunga nyimbo zinazopendwa duniani kote. Februari 1962 Bob alirekodi nyimbo 4, Judge Not, One Cup of Coffee, Do You Still Love Me? na Terror, producer wake Leslie Kong, akaziingiza sokoni japo wimbo wa One cup of coffee uliingizwa sokoni na kutambulishwa kwa kutumia ‘aka’ ya Bobby Martell. Mwaka 1963, Bob Marley, Bunny Wailer, Peter Tosh, Junior Braithwaite, Beverley Kelso, and Cherry Smith wakaanzisha kundi lao wakajiita The Teenagers baadae wakabadili jina na kujiita The Wailing Rudeboys, hatimae wakajiita The Wailing Wailers, jina ambalo wengi hulifahamu. Na wakati huu ndipo wakagundulika na producer Coxsone Dodd wakarekodi wimbo wa Simmer Down na wimbo huu ukapanda mpaka namba 1 katika top ten ya Jamaica na kufikia February 1964 na uliweza kuuza nakala 70,000 wakati huo.
The Wailers likawa kundi lilioanza kuingia studio mara nyingi sasa na hata kushirikiana na wanamuziki waliokuwa maarufu wakati huo. Kufikia mwaka 1966, wanamuziki kadhaa wakawa wameliacha kundi hilo na kuwaacha vigogo watatu wakiendeleza kundi nao ni Bob Marley, Bunny Wailer, and Peter Tosh. Mwaka 1966 Bob akamuoa Rita Anderson na kuhamia kwa muda Marekani katika jiji la Delaware, na kwa wakati mfupi alifanya kazi katika kiwanda cha kutengenza magari cha Chrysler akijiita Donald Marley. Pamoja na kuwa alizaliwa na kulelewa kama Mkatoliki Bob taratibu akaanza kuingia katika imani ya kiRastafari. Aliporudi tena Jamaica akaingia rasmi katika Urastafarian na kuanza kufuga nywele kwa mtindo wa dreadrocks. Imani hii ya kufuga nywele bila kukata inatokana na maandiko kuhusu Samson kwenye biblia, ambaye inaelezwa siri ya nguvu zake ilikuwa katika nywele, na alipokatwa nywele nguvu zote zilimuishia.

Rais Obama kwenye Makumbusho ya Bob Marley


Kipindi hichohicho baada ya kurudi Jamaica, kulitokea ugomvi kati ya wanamuziki na producer Dodd kuhusu pesa, Marley na wenzie wakaungana na producer mwingine Lee “Scratch”, na kurekodi nyimbo ambazo wachunguzi husema ndizo nyimbo bora zilizowahi kurekodiwa na Wailers. Kati ya mwaka 1968 na 1972, Bob, Rita Marley, Peter Tosh na Bunny Wailer walirudia nyimbo kadhaa za Wailing Wailers, japokuwa Bunny baadae alikuja kusema nia ya nyimbo hizo ilikuwa ziwe ‘demo’ tu kwa record labels ili kujitambulisha.

Sanamu ya Bob Marley Kingston Jamaica

 Mwaka 1972 Wailers waliingia mkataba na kampuni ya CBS ya London, na kuanza ‘tour’ ya Uingereza wakisindikizana na muimbaji maarufu Johnny Nash. Wakiwa London walimuomba road manager wao kuwatambulisha kwa Chris Blackwell, ambae kamouni yake ya Island Records iliwahi kusambaza nyimbo zao fulani za zamani, hivyo walitaka kuongea nae kuhusu malipo yao ambayo kwa kweli yalikuwa ni Pauni chache tu, matokeo ya kuonana na huyu bwana ikawa ni Wailers kupata advansi ya Pauni za Kiingereza 4000 ili kutengeneza album. Katika kipindi hichohicho Jimmy Cliff alikuwa kaondoka kwenye mkataba na Island Records na hivyo kampuni hiyo ilikuwa inasaka wasanii wa kuchukua nafasi ile. Wailers waliporudi Jamaica wakarekodi album ya Catch a Fire. Catch a Fire ndio ilikuwa album ya kwanza ya Wailers na ilianza kusambazwa mwezi April 1973. Iliuza album 14,000, mauzo haya hayakuwafanya Wailers kuwa masupastaa lakini yalifanya watu waanze kuwaulizia. Katika album hiyo kulikuweko na wimbo I shot the sheriff, mwanamuziki Eric Clapton aliusikia wimbo huo kutoka album aliyopewa na rafiki yake, akaurecord kwa stail yake, ukatokea kupendwa sana Marekani na kufika namba 1 kwenye Billboard Hot 100 tarehe 14 Septemba 1974. Mwaka 1974 Wailers ikavunjika Bunny, Peter Tosh na Bob Marley kila mmoja akaanza kufanya kazi kivyake. Japo Bob aliendelea kurekodi kwa jina la Bob Marley and the Wailers akiwa na wasanii kama Carlton Barret kwenye drums na nduguye Aston “Family Man” Barrett kwenye gitaa la bezi, Junior Marvin na Al Anderson kwenye gitaa la solo, Tyrone Downie na Earl “Wya” Lindo kwenye keyboards, Alvin “Seeco” Patterson akiwa kwenye percussion. Wale mabinti “I Threes” Judy Mowatt, Marcia Griffiths, na Rita Marley mke wa Bob. Wakiwa kwenye sauti za kujibu. Mwaka 1975, wimbo wa “No Woman, No Cry” uliokuwa katika album ya Natty Dread ukaweza kuingia katika chart za nchi nyingine nje ya Jamaica, mwaka 1976 album ya Rastaman Vibration ikaweza kupenya kuingia soko la Marekani na kufika katika nyimbo bora 50 za Billboard Soul Charts. Siku ya Desemba tarehe 3 mwaka 1976, siku mbili kala ya tamasha ambalo Michael Manley Waziri Mkuu wa Jamaica alikuwa ametayarisha ili kupunguza uhasama kati ya makundi mawili makubwa ya kisiasa, Bob Marley akiwa nyumbani kwake na mkewe na meneja wake Don Taylor, ghafla wakaingia watu na silaha na kumwaga risasi, mke wa Bob na meneja walipata majeraha makubwa lakini hatimae waliweza kupona, Bob alipata majeraha madogo kifuani na kwenye mkono. Inasadikiwa zilikuwa ni njama za kisiasa. Tamasha liliendelea na Bob alishiriki akiwa na vidonda vyake, alipoulizwa akajibu, “The people who are trying to make this world worse aren’t taking a day off. How can I?” Wanamuziki wenzie wa Wailers wote walijificha kuogopa kifo, bendi ya Zap Pow ndio ilimpigia muziki siku hiyo, watu kama 80,000 walihudhuria onyesho hilo.

Mwaka 1976 Marley aliondoka Jamaica, akahamia Uingereza kati ya mwaka 1977 mpaka 1978. Alipokuwa Uingereza ndipo akarekodi album mbili Exodus na Kaya. Exodus ilikuwa kwenye chart za Uingereza kwa wiki 56, yaani mauzo yake yalikuwa kati ya album bora kwa wiki 56. Inasemekana aliuza nakala milioni 75 za album hiyo. Mwaka 1978 alirudi tena Jamaica kufanya concert jingine la amani lililoitwa One Love Peace Concert, mwisho wa onyesho, kwa maombi ya Bob viongozi wa kisiasa waliokuwa wakipingana na kupelekea wafuasi wao kuuwana, Michael Manley ( kiongozi wa chama kilichokuwa kikitawala wakati huo People’s National Party) na Edward Seaga (kiongozi wa upinzani wa cham cha Jamaica Labour Party), wakashikana mikono.
Bob alirekodi kwa jina la Bob Marley and the Wailers album 11, album nne za live na saba za studio, ikiwemo Babylon by Bus.

 July 1977, Marley akakutwa na kitu kimeota chini ya ukucha wa kguu wake, kitu kilichoonekana na madaktari kuwa ni aina ya cancer, hivyo daktari wake akmshauri akatwe kidole, Bob akakataa kwa maelezo kuwa dini yake hairuhusu. Mwezi May 1980 bendi ilikuwa imeamilisha ‘tour’ ya Ulaya ambapo ilipofika Milan Italy ilifanya onyesho lililohudhuriwa na watu 100,000, alipomaliza Ulaya akaenda Marekani akafanya show mbili Madison Square Garden, tour hizo zilipewa jina la Uprising Tour. Tarehe 23 September 1980 Bob alifanya onyesho lake la mwisho kwani afya yake ikaanza kudorora haraka sana, ile kansa ya kidoleni ilikuwa imesha sambaa mwili mzima, kwa miezi minane alikuwa hospitali. Bob alifariki katika hospitali ya Cedars of Lebanon Hospital tarehe 11 Maty 1981 akiwa na umri wa miaka 36 tu. Kilichomuua ni kansa kuingia katika ubongo maneno yake ya mwisho kwa mwanae Ziggy ni “Money can’t buy life.” Yaani PESA HAZIWEZI KUNUNUA MAISHA. Bob Marley alizikwa jirani na alipozaliwa tarehe 21 May 1981, kwa mazishi ya Kitaifa na kadri ya imani yake ya Urastafarian. Bob alizikwa na gitaa lake la jekundu la aina ya Gibson Les Paul.

MIAKA 36 BAADA YA KIFO CHAKE MFALME WA MZIKI WA REGGAE (BOB MARLEY) MIAKA 36 BAADA YA KIFO CHAKE MFALME WA MZIKI WA REGGAE (BOB MARLEY) Reviewed by CONVIDA FUNERAL HOME COMPANY LIMITED on 8:25 AM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.