banner image

Nimepigana dhidi ya utawala wa watu weusi na nimepigana dhidi ya Utawala wa watu weupe – Nelson Mandela.



Mnamo mwaka 1964 katika kizimba cha mahakama ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, katika Mji wa Johanesburg alikuwa amesimama shujaa, akiwa anasubiri hukumu yake, kwangu naiita ‘hukumu ya kihistoria’



Alikuwa tayari kwalolote kwa maisha yake  binafsi lakini kwa  faida ya maisha ya watu wote  wa Taifa la Afrika Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla bila Kujali alikuwa ni Mwafrika au mtu mweupe, mtoto, kijana au mzee mwanamke au mwanaume ili mradi tu haki, uhuru na usawa kwa wote vitimie.


Akiwa tayari ameshatumikia kifungo cha miaka miwili jela kwa kipindi hicho na huku akisubiri hukumu katika kesi  yake nyingine iliyojulikana kama “ The Rivonia Trial” na huku akikabiliwa na hukumu ya kifo, maneno yake kwa mahakama katika hotuba yake maarufu inayojulikana kama “ Speech from The Dock” mnamo tarehe 20 Aprili 1964 Nelson Mandela alisema
“Nimepigana dhidi  ya utawala wa watu weupe na nimepigana dhidi ya utawala wa watu weusi. Nimekuwa  nikiitetea dhana ya demokrasia na jamii huru ambayo watu wote wataishi kwa amani na fursa sawa. Ni dhana ambayo nina matumaini ya kuishi nayo na kuitimiza. Basi ikibidi ni dhana  ambayo nimejiandaa kufa nayo”
Nelson Rolihlahla Mandela alitoa maneno haya kutoka moyoni  na akimaanisha kuwa yeye ni jasiri na yuko tayari kwa mapambano ya vitendo dhidi ya ubaguzi wa rangi.



Siku ya leo tarehe 05 Desemba, 2016, ni miaka mitatu tangu alipofariki, lakini historia yake, maneno yake, harakati zake na matendo yake yanaishi na kujidhihirisha nchini  Afrika ya Kusini, Afrika na Dunia kwa ujumla.
“Kama binadamu alifanya ambayo aliona ni jukumu lake kwa watu wake na nchi yake anaweza akapumzika kwa amani. Naamini nimefanya juhudi hizo na hiyo ndio maana itanifanya nilale milele”- Mandela
Mwenyezi Mungu ana haki ya kumlaza na kumpumzisha kwa amani na milele Mandela, hakuyumbishwa na hali zozote na wala na mtu yeyote, ni kweli alitimiza jukumu lake. Jukumu la kupigana dhidi ya  utawala wa kimabavu, uonevu, ukandamizaji, ubaguzi wa rangi si kwa Afrika kusini tu! La hasha Ushindi wake ulikuwa ni wa dunia nzima.
 Tupendane kila mmoja wetu kama tulivyompenda yeye. Tumsherekee Madiba, kwa pamoja na tusimuangushe” Askofu Desmond Tutu

Aliendelea Kusema  Askofu Desmond  Tutu, “ Kwa karibia zaidi ya miaka 27 Madiba alitufundisha jinsi ya kuungana , kuwa pamoja na kuaminiana  katika  kila mmoja wetu. Alikuwa ndio alama ya umoja   wetu tokea muda alipotoka jela.
Katika hotuba yake ya Cape Town,
Ilikuwa Februari 1990, ambapo Mandela alikuwa ndio ameaachiwa kutoka jela, alitoa hotuba yake ya kwanza katika muda wa  kipindi cha miaka 27, eneo la parade mji wa Cape Town.

 Alimalizia hotuba yake kwa maneno  yale yale aliyomalizia katika hotuba yake ya mnamo mwaka 1964—akiamini yuko tayari kujiandaa kufa kwa kile anachokisimamia.
Katika hotuba yake hiyo ya kuimarisha mapamabano, Mandela aliendelea kusema
“ Tumeusubiria uhuru wetu kwa muda mrefu sana. Hatuwezi kusubiri tena, sasa ni muda wa kuimarisha mapambano katika pande zote, kupumzisha juhudi zetu litakuwa ni kosa kwa vizazi vyetu vinavyokuja na hawatakuwa tayari kutusamehe.…… Tunawaita ndugu zetu weupe wajiunge nasi pamoja katika kutengeneza Afrika Kusini mpya”.
Je nani angeweza kumtaka adui yake aungane nae pamoja? adui aliyekunyima, kukukandamiza na kukukatili uhuru wako wa zaidi ya robo ya maisha yako  kwa kukufungia gerezani akikutenga na mke wako, watoto, ndugu na wananchi  unaowapigania. je nani mwenye moyo na imani hiyo?  

 Askofu Desmond Tutu katika hotuba yake ya kumuaga rafiki yake Nelson Mandela ambapo alizoea kumuita kwa jina la Madiba, mnamo Desemba 2013 aliuliza ‘Je Madiba alikuwa mtakatifu? basi kama hakuwa mtakatifu, alikuwa hana dosari! naamini alikuwa ana utakatifu kwa sababu aliwahamasisha  watu wengi na alionesha tabia yake kwa uwazi na sifa nyingi nzuri ambazo mungu anapendezewa nazo  kama huruma, kuwajali wengine, kuwa mtu mwenye kuhitaji amani, misamaha na maridhiano hakika alijaliwa kuwa nazo.
Naamini katika siku ya leo ambapo tunamkumbuka shujaa wetu, Jasiri, Mpigania haki za binadamu  Nelson Mandela, Afrika na dunia ina  viongozi wachache sana wenye haiba yake au  hakuna hata mmoja ambaye naweza sema ni Nelson Mandela  wa leo!
Mandela alikufa nyumbani kwake Johannesburg tarehe 05 Desemba, 2013.
“ Taifa letu limepoteza mtoto wake mkubwa wa kiume, watu wetu wamepoteza baba yao alisema Rais wa Afrika Kusini Jacob Zumma wakati akihutubia Taifa kupitia Telivisheni, katika Alhamisi ya kifo cha Mandela








“Nelson Mandela  amefikia mafanikio makubwa kuliko ilivyotarajiwa na mtu yoyote.” Alisema Rais Barack Obama aliendelea kusema tumempoteza mmoja wa mtu maarufu, jasiri na binadamu ambaye kila mmoja wetu atamuelezea katika maisha yake "
 Rolihlahla Mandela  alizaliwa katika ukoo wa Madiba kijiji cha Mvezo jimbo la Transkei tarehe18 July 1918. Mama yake alikuwa Nonqaphi Nosekeni na baba yake alikuwa Nkosi Mphakanyiswa Gadla Mandela, baba yake alikufa alipokuwa na miaka 12
 Alihudhuria  masomo ya shule ya msingi huko  Qunu, ambapo mwalimu wake Bi Mdingane, alimpa jina la  Nelson,  kwa mujibu wa  taratibu za wakati huo watoto wote wa shule lazima wapewe majina ya kikristo .
Nelson Mandela alifanikiwa kumaliza degree ya kwanza ya Sanaa (B.A) mwaka 1943 katika Chuo kikuu cha Afrika Kusini baadae alijiunga na masomo ya digrii ya kwanza ya Sheria (LLB) katika Chuo cha Witwatersrand, lakini alishindwa kuendelea akaanza tena kusoma kupitia  Chuo Kikuu cha London baada ya kumaliza kifungo  mwaka 1962 lakini hata hivyo hakumaliza.
Mwaka 1989, akiwa katika miaka yake ya mwisho ya kifungo alihitimu shahada ya kwanza ya sheria katika Chuo Kikuu cha South Africa
Mandela alianza kujihusisha na siasa miaka ya  1942, alijiunga na African National Congress (ANC)  mwaka 1944 alishiriki katika kuanzisha umoja wa vijana wa  ANC ( ANCYL)
Mwaka 1944 alimuoa binamu wa Walter Sisulu’s , Evelyn Mase, ambaye alikuwa nesi. Wakapata watoto wa kiume wawili, Madiba Thembekile "Thembi" and Makgatho, na watoto wa kike wawili wote waliitwa Makaziwe, wa kwanza alifariki akiwa bado mdogo. Waliachana na mke wake mnamo mwaka 1958.
Mandela aliibuka kushika nyadhifa mbalimbali za kisiasa na kukutana na misukosuko ya utawala kibaguzi wa rangi  wa makaburu nchini Afrika kusini ambapo mnamo mwaka 1952 yeye na wenzake 19 walishtakiwa na kuhukumiwa kwa makosa ya kuipinga serikali ya kibaguzi.
Mnamo tarehe 14 Juni mwaka 1958 Mandela alimuoa Afisa Ustawi Winnie Madikizela,  walifanikiwa kuzaa watoto wawili wa kike   Zenani na Zindziswa, waliachana  kwa talaka mwaka  1996.
Tarehe 11 Juni 1964 Mandela na wenzake saba Walter Sisulu, Ahmed Kathrada, Govan Mbeki, Raymond Mhlaba, Denis Goldberg, Elias Motsoaledi and Andrew Mlangeni, walihukumiwa kifungo cha maisha na kupelekwa gereza lililopo katika kisiwa cha Robben Island.


Siku ya jumapili tarehe 11 Februari 1990,  siku tisa baada ya kuhurusiwa tena kwa vyama vya  ANC na PAC Mandela aliachiwa huru kutoka kifungo.

Mnamo mwaka 1993 pamoja na Rais  FW de Klerk kwa pamoja walipewa Tuzo ya Amani ya Nobeli na tarehe  27 Aprili 1994 alipiga kura kwa mara ya kwanza katika maisha yake akitimiza ndoto yake kwa kile ambacho alikisimamia na kuwa tayari kufa kwa ajili yake kama alivyosema  katika hotuba yake ya mwaka 1952.

Nelson Rolihlahla Mandela Madiba akawa Rais wa kwanza wa Taifa huru la Afrika Kusini ‘ Rainbow Nation”  aliechaguliwa  kidemokrasia  mnamo tarehe 10 Mei, 1994.

 Katika siku yake ya kuzaliwa akiwa anatimiza miaka 80 alimuoa Graca Machel akiwa ni mke wake wa tatu.

Akitimiza ahadi yake mwaka 1999 baada ya kipindi kimoja cha kuwa Rais , aliamua kuachia ngazi.

Mnamo mwaka 2009, Umoja wa Mataifa unatangaza kuwa   Julai 18 ni “Nelson Mandela International Day” in kwa ajili ya kutambua mchango wake katika demokrasia, uhuru, amani na haki za binadamu duniani kote.

Nelson Mandela aliweza kuandika vitabu mbali mbali vikielezea maisha yake binafsi na harakati za kupinga serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini.  Vitabu hivyo ni kama “ Long Walk to Freedom-1995”,  No Easy Walk to Freedom -1990,  na the Struggle is my Life -1978

Kwa lugha ya kiingereza maneno yake haya  yenye kutia matumaini, moyo, ujasiri na muendelezo wa mapambano kwa jamii ambazo bado zinaishi katika zama za za uonevu na ubaguzi yanahitimisha siku hii ya kumbukumbu “the greatest glory in living lies not in never falling but in rising every time we fall." - Nelson Mandela

Mwenyezi Mungu aendelee kumlaza mahali pema peponi  Nelson Rolihlahla  Madiba Mandela 

 

Long live South Africa – Viva!     Long live Mandela- Viva !

Nimepigana dhidi ya utawala wa watu weusi na nimepigana dhidi ya Utawala wa watu weupe – Nelson Mandela. Nimepigana dhidi ya utawala wa watu weusi na nimepigana dhidi ya Utawala wa watu weupe – Nelson Mandela. Reviewed by CONVIDA FUNERAL HOME COMPANY LIMITED on 6:33 PM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.