banner image

“Kila mtu sasa anakubali ubaguzi wa rangi ulikuwa ni kitu kibaya, kikubwa nilichofanya nilieleza yote, watu walitaka kujua vipi tulivyoweza kuishi Afrika Kusini ( South Africa).



Nilichofanya niliiambia dunia ukweli na kama ukweli wangu uligeuka kuwa siasa, siwezi kufanya chochote juu ya hilo”, Maneno  haya aliyanena Mama wa Africa Miriam Makeba Mwanamuziki nguli wa  Afrika Kusini na Mtetezi wa haki, ambaye ndie alikuwa Mwanamuziki wa kwanza   Afrika kuufanya muziki wa afrika kuwa maarufu duniani.

“Miriam Makeba ni nyota ya Afrika ambayo inangaa hadi leo, ikitoa mwanga wa matumaini , nguvu na ujasiri wa kupambana katika  maisha , “hii ni hadithi ya gwiji” kama anavyoelezea Niyi Coker Profesa  wa Chuo  Kikuu cha Missouri–St. Louis  Marekani, katika idara ya sanaa, maonesho ya Jukwaani na utengenezaji filamu wakati akitengeneza filamu ya” Miriam Makeba: Mama Africa Musical”  , Niyi Coker aliendelea kumzungumzia hayati Miriam Makeba kwa kusema, “Miriam alipoteza vitu vingi sana  vya kibinafsi, fedha kwa kufanya yale ambayo aliamini anaweza na kuyasimamia hasa katika kupambana na ubaguzi wa rangi kitu ambacho kilipelekea mpaka kufukuzwa nchini Marekani.
Katika Maelezo yake siku ya Jumatatu ya Kifo cha hayati  Miriam Makeba. Mpigania uhuru, Mpinga ubaguzi wa rangi, mwanaharakati na mtetezi haki  za kibinadamu na Raisi wa zamani Taifa huru dhidi ya ubaguzi wa rangi la Afrika Kusini, Nelson Mandela alieleza kuwa “ Mpendwa wetu Miriam ametutia majonzi makubwa sisi na Taifa kwa ujumla, sauti  yako tamu ilitoa matumaini kwa watu waliokuwa wanaishi uhamishoni na katika hali za kutapa tapa kutokana na ubaguzi wa rangi nchini afrika kusini, muziki wako ulitupa nguvu ya matumaini kwetu sisi wote. Kwa hakika ndie alikuwa mwanamke namba moja wa Afrika Kusini mwenye utajiri wa upendo na kutetea haki za binadamu  kwa hakika alistahili kuitwa  Mama Afrika, Mama wa mapambano kwa Taifa letu la Afrika Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla” alimalizia Mandela

Miriam Makeba alifariki ghafla katika mji wa  Castel Volturno nchini Italia akiwa na umri wa miaka 76 baada ya kutoka kushiriki kuimba katika tamasha la muziki lililoandaliwa nchini Italia mahsusi kumsaidia mwandishi Roberto  Saviano  katika mapambano dhidi ya makundi ya uhalifu kutokana na maandiko yake juu ya kupinga mipango ya kiuhalifu  iiliyokuwa ikifanywa na na kundi la Cammora lenye mlengo wa kimafia katika mji wa Campania nchini Italia. Miriam hakupenda uonevu wa aina yoyote na hicho hasa  ndicho kilichomsukuma “Mama Afrika” kwenda kushiriki kuimba kwenye tamasha hili  akiamini kuwa  kupitia muziki sauti yake itapaa na kupeleleka matumaini kwa wahanga wa uonevu, hivyo Miriam alifariki akiwa katika mapambano.
Taarifa ya Daktari ilieleza kuwa Mama wa Afrika amekufa kutokana na mshutuko wa moyo saa chache tu alipotoka kuhitimisha onesho ambalo lilikuwa  la mwisho katika maisha yake ya ulimwengu, mnamo tarehe 10 Novemba, 2008. Dunia ilipata mshutuko mkubwa kutokana na msiba huu. Maisha ya kutumia sauti yake nzuri aliyojaliwa na Mwenyezi Mungu  kwa ajili ya kutoa matumani kwa jamii zilizokuwa zinaishi katika unyanyasaji, uonevu, ubabe, umasikini na kila ya aina ya dhuluma. Ndio ! ilikuwa ni mwisho wa maisha ya Miriam Ulimwenguni lakini sio mwisho wa fikra zake, mapambano na utetezi wake, hivi vyote vinaendelea kuishi katika ulimwengu wa leo na kesho.

Miriam “ Zenzi” Makeba alizaliwa tarehe 04 Machi, 1982 katika mji mdogo ndani ya viunga vya jiji la Johannesburg  baba yake aliitwa Caswell, kutoka kabila la Xhosa, mama yake aliitwa Christina, wa kabila la Swazi , Jina la Zenzi katika maana ya  kabila la Xhosa Uzenzile ni kuwa  “ haina haja ya kumlaumu mtu kwa matatizo yako” lilikuwa ni jina la kitamaduni, likimaanisha kupambana na kutoa msaada katika matatizo ya kimaisha, Baadae familia yake ikahamia mji wa Transavaal ambapo baba yake alikuwa anafanya kazi kama karani katika kampuni ya shell wakati mama yake akifanya kazi za uponaji kiimani kwa maana ya uganga wa kinyeji  pamoja na za majumbani.
Baba yake  alifariki  akiwa mdogo, hii ilimlazimu Miriam kufanya kazi za ndani lakini alikuwa ameshagundua”  muziki ni mojawapo ya maajabu” ambayo yanaweza kumsaidia kujikwamua kutoka katika umasikini. Safari ya muziki ya zaidi ya miongo minne ya Miriam Makeba ilianzia hapa, akiwa kijana alianza kusikiliza miziki ya kina Ella Fitzgerald na Billie Holiday. Kaka yake Joseph ambaye alikuwa ni mpiga tarumbeta na piano ndie aliemtabulisha katika ulimwengu muziki wa Jazz wa kimarekani, alipokuwa akiimba na  kaka yake  Miriam  anakumbuka kwa kuelezea “Saa zingine nilikuwa sijui nasema nini lakini niliweka akili na nguvu zangu zote “ (Makeba na Hall 1987,21).


Miriam alijifunza muziki kupitia kuimba na wanamuziki wengine kupitia bendi za muziki mbalimbali nchini Afrika kusini alianza na Bendi ya Mpwa wake iliyokuwa inaitwa Zweli band, “The Cuban Brothers” mpaka kufikia kuanza kufanya kazi ya kwanza ya kulipa katika miaka ya 1940 hadi 1950 akiwa na kundi maarufu la Manhattan Brothers na hapa ndio safari yake ya kwenda ulaya ilipoanzia kwani kupitia kundi hili walitengeneza nyimbo iliyotumika katika sinema iliyotayarishwa na Lionel Rogosins iitwayo “Come Back, Africa (1959). Rogosin Mtayarishaji wa kimarekani alikuwa ameiona sauti ya dhahabu katika Afrika, hakufikiria mara mbili aliondoka na Miriam pamoja filamu kuelekea London.

Akiwa London Miriam Makeba alikutana na Harry Belafonte ambaye walikutana wakati wa uandaaji wa filamu ya “Come Back, Africa” rudi Afrika, katika muda usiojulikana Belafonte alimfanyia mpango Miriam kuingia nchini marekani akiwa na umri wa miaka 27. Lilikuwa ni jambo la kushangaza katika wiki ya kwanza Miriam alishiriki katika onesho la Steve Allen jijini Los Angeles, vyombo vya habari vikaanza kumfananisha na  Ella Fitzgerald, Ethel Merman na Frank Sinatra. Nyimbo za Miriam zikaanza kupata umaarufu mkubwa, baadhi ya nyimbo zake maarfu  ni Qongqothwane iliyojulikna kwa lugha ya kiingereza  “The Click Song,” na nyingine kama “Pata Pata,” sangoma  na zingine nyingi tu. Akiwa marekani alifanya ziara mbali mbali za kimuziki zenye mafanikio aliimba katika siku ya kuzaliwa ya Raisi wa Marekani John F. Kennedy mnamo mwaka 1962, alitunukiwa Tuzo za Grammy akiwa na Belafonte mnamo mwaka 1965, pamoja na kushiriki katika tamasha la muziki nchini Zimbabwe mnamo mwaka 1987, Tamasha la kutimiza miaka 70 ya kuzaliwa Nelson Mandela nchini uingreza katika uwanja wa Wembley mnamo tarehe 11 Juni 1988, aidha alishiriki kuburudisha katika pambano maarufu la ndondi ulimwenguni kati ya Mohamad Ali na George Foreman lililofanyika nchini Zaire lililojulikana kama “ Rumble in the Jungle” Muziki wa Miriam pamoja na sauti yake yenye kujaa matumaini, nguvu na ujasiri wa kupambana ilipenya kwenye masikio ya walimwengu huku ikiamsha ari ya kujitambua na kuleta burudani ambayo haina kifani.
Pamoja na mafanikio ambayo alikuwa ameyapata katika muziki nchini marekani na ulimwenguni kote Miriam aliutunza na kuendeleza uasili wa urembo wa kiafrika kwa kutotumia vipodozi vya aina yoyote na wala kuweka dawa katika nywele zake na hii ilifanya  kuwepo kwa mtindo maarufu duniani uliojulikana kwa jina la kiingereza kama “Afro look”

Miriam Makeba aliishi uhamishoni kwa kipindi cha muda wa zaidi ya miaka 30 katika nchi mbali mbali za bara la Afrika na Ulaya kutokana na msimamo wake wa kuipinga serikali ya kibaguzi ya afrika kusini iliyokuwa chini ya utawala wa makaburu. Serikali ya ubaguzi wa rangi ya afrika kusini  ilizuia kupigwa kwa nyimbo zake pale baada ya  kutoa hotuba katika mwaliko wa  Kamati Maalum ya Umoja wa mataifa ya kupinga ubaguzi  mnamo tarehe 16 Julai,1963,  Miriam alisema “ Nchi yangu imegeuzwa kuwa gereza kubwa na serikali ya kimabavu, hivyo nauomba Umoja wa Mataifa, kitu cha kwanza kabisa waweke pingamizi la kusafirishwa kwa silaha, bila kuwa na shaka hata kidogo naamini kuwa silaha hizi zitatumika dhidi wanawake wa afrika na watoto.” Miriam Alipewa Tuzo nyingi za kiheshima kimataifa kuanzia ile ya amani ya Umoja wa Mataifa ya Dag Harmmaskjold mnamo mwaka 1986 na nyingine nyingi.
Katika maisha yake binafsi Miriam alipata kuolewa na wanaume mbali mbali kuanzia Stokley Carmichael ambaye alikuwa mwanachama wa kikundi cha “Black Panther”  mwaka 1968 ndoa hii ilimletea matatizo na hivyo kupelekea kuzuiwa kuendelea na shughuli za kimuziki nchi marekani, aidha pia alipata kuolewa na Mpiga Tarumbeta  wa Afrika Kusini Hugh Masekela. Mwenyezi Mungu alimjalia kupata mtoto wa kike Bongi ambaye baadae alifariki dunia.
Vijana wengi wa Afrika Kusini na Dunia kwa ujumla hawajui Miriam Makeba alikuwa nani na alipigania nini lakini wakati anatangaza kuachana na muziki mnamo mwaka 2005 akaja kugundua kuwa bado alikuwa maarufu duniani akisema ”  Kila mtu alinitafuta na kuniambia njoo uje utuambie kwaheri”  Miriam Makeba “Mama Afrika”  aliwaaga washabiki wake na ulimwengu kwa ujumla akiwa jukwaani  pale nchini Italia wakati  akiwatetea wanyonge wa Italia kupitia muziki wake,  miaka nane imepita sasa tangu Mwenyezi Mungu amuite Miriam na kumwambia imetosha umefanya kazi kubwa sana pumzika, lakini bado nabaki kujiuliza maswali  kwanini Robert Saviano alimtaka Miriam aende Italia ? kwa uhalifu unaofanywa na kundi la Kimafia la Italia. Akili yangu inaniambia Miriam alikubali kwa  sababu  alijitambua na alikuwa haogopi kueleza na  kushiriki katika ukweli na kutoa matumani kwa wanyonge kama alivyowahi kusema katika maneno yake “ kuna vitu vitatu nimezaliwa navyo katika hii dunia ambavyo nitakuwa navyo mpaka mwisho wa maisha yangu navyo ni matumaini, kujitambua na nyimbo”
Alikuwa ni rafiki yake Philemon Hou, mwanamuziki mwenzake wa Afrika kusini ambaye alimfundisha Miriam  shairi ambalo mara nyingi alikuwa akisoma pamoja na wajukuu zake mpaka umauti ulipomkuta
                                    Sisi ni watu wa Afrika
                                    Mtu wa Afrika!
                                    Mtu wa Afrika!
                                    Sisi ni watu wa Afrika
                                    Na wala usisahau!


Mwenyezi Mungu aendelee kukulaza mahali pema peponi shujaa wetu, mama yetu wa afrika, mpiganaji na Mkombozi, bado naiona nuru yako ikiangaza na kumulika ullimwenguni kote na kutoa matumaini kwa wanyonge
Viva Afrika

Viva Miriam Makeba, Aluta Continua!
“Kila mtu sasa anakubali ubaguzi wa rangi ulikuwa ni kitu kibaya, kikubwa nilichofanya nilieleza yote, watu walitaka kujua vipi tulivyoweza kuishi Afrika Kusini ( South Africa). “Kila mtu sasa anakubali ubaguzi wa rangi ulikuwa ni kitu kibaya, kikubwa nilichofanya nilieleza yote, watu walitaka kujua vipi tulivyoweza kuishi  Afrika Kusini ( South Africa). Reviewed by CONVIDA FUNERAL HOME COMPANY LIMITED on 4:05 PM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.